BREAKING NEWS

Wednesday, July 13, 2022

JEZI FEKI ZA SIMBA NA YANGA ZANASWA MWANZA

 




Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limekamata jezi feki dazani 296 za Simba na Yanga zikiuzwa na wafanyabiashara huku wito ukitolewa   kwa wauzaji kuuza bidhaa halali ili kutohujumu mapato ya klabu hizo.


Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza leo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhan Ng'anzi amemtaja aliyekamatwa na bidhaa hizo ni mfanyabiashara, Said Furaha (31) mkazi wa Nundu.


Amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 5 saa 12:30 mchana eneo la barabara ya Pamba sokoni wilaya ya Nyamagana kwa kosa la kupatikana na jezi bandia dazani 145 zenye nembo ya klabu ya Simba zinazomilikiwa na Kampuni ya Vunjabei na jezi dazani 151 zenye nembo ya Yanga zinazomilikiwa na Kampuni ya GSM, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.



"Jeshi letu linaendelea na upelelezi wa kina kuhusiana na shauri hili ili kubaini mtandao mzima wa wahusika wote wanaotengeneza, kuagiza na kuingiza nchini bidhaa hizo bandia, ambapo inapelekea wadhamini wa klabu hizo kukosa mapato," amesema Ng'anzi.


Kwa upande wake, Mshauri wa kampuni ya GSM tawi la Mwanza, Mahsen Omar ameomba mamlaka kuhakikisha watuhumiwa wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kukomesha tabia hizo.



Meneja wa Vunjabei Kanda ya Ziwa, Said Malekela amelishukuru jeshi la polisi na kuomba hatua zaidi kuendelea kuchukuliwa huku akiwataka mashabiki wanaonunua jezi za klabu ya Simba kutambua bidhaa halali zenye nembo ya timu hiyo na ile ya Vunjabei.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates