BREAKING NEWS

Wednesday, July 6, 2022

MAJALIWA:MADINI YA BUNYU (GRAPHITE) KUANZA KUCHIBWA RUANGWA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Chunyu wilayani Ruangwa baada ya kutembelea Shule ya Msingi Chunyu, Ju (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo katika majadiliano na kampuni ya Uranex kwa ajili ya ujenzi wa mgodi wa madini ya bunyu (graphite) utakaoanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa wananchi wa wilaya ya Ruangwa wajiandae kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zitokanazo na ujenzi wa mgodi wa graphite.

Ameyasema hayo  wakati akizungumza na wananchi katika vijiji vya Namikulo, Namkatila na Matambarale katika kata ya Chunyu wilayani Ruangwa, Lindi.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kila kwenye rasilimali kabla ya kuanza uwekezaji lazima wahusika wajadiliane na Serikali ili kubaini namna ambavyo itanufaika.”

Waziri Mkuu amesema wakazi wa maeneo hayo watakuwa ndio wanufaika wa kwanza kutokana na shughuli mbalimbali zinakazokuwa zikiendelea kuanzia hatua ya ujenzi hadi uzalishaji.

“Kila shughuli itakayofanyika hapa ni fursa kwetu sisi wana-Namikulo na wana-Ruangwa kiujumla. Tujipange sawa sawa Serikali yenu ipo makini kuhakikisha mnanufaika na mradi huo.”

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa kampuni ya Uranex, Mhandisi Isaac Mamboleo amesema kampuni yao inatarajia kuanza ujenzi wa mgodi huo katika mwaka huu wa fedha.

Amesema mradi huo ambao utahusisha vijiji saba unatarajia kugharimu shilingi bilioni 625 na utazalisha ajira 950 kati yake ajira 600 wakati wa ujenzi na ajira 350 wakati wa uzalishaji.

Mhandisi Mamboleo amesema kwa sasa wanakamilisha ujenzi wa nyumba 59 zenye gharama ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kuwafidia baadhi ya wananchi waliopisha ujenzi wa mradi huo.

Amesema baada ya kukamilisha ulipaji fedha kama fidia ya ardhi na mazao, pia wanajenga nyumba zenye ubora kwa ajili ya kuwafidia wananchi 59 waliokuwa na nyumba katika eneo la mradi. “Nyumba hizo tunajenga nje ya eneo la mradi na kila mtu anajengewa nyumba kulingana na ukubwa wa nyumba yake ya awali.”

Nao, baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wameziomba kampuni za uwekezaji zitoe kipaumbele kwa wananchi wanaoishi karibu maeneo ya mradi na kwamba wamejipanga na wako tayari kwa kazi

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mihewa wakaimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowasalimia akiwa katika ziara ya wilaya ya Ruangwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates