CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa
taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha na Uchumi na Mbunge wa Kalenga, Dkt.
William Mgimwa ambaye amefariki akiwa kwenye matibabu Afrika Kusini.
Kwa
masikitiko makubwa CHADEMA kinatuma salaam za pole kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa kuondokewa na msaidizi wake wa karibu
na mtumishi mwenzake serikalini.
Chama
kinatoa salaam za dhati kwa familia ya marehemu Mgimwa kwa kuondokewa na baba
na mpendwa wao, katika wakati ambao tunaamini walikuwa bado wakimhitaji sana kama
moja ya nguzo za familia.
CHADEMA pia
inatuma salaam za pole kwa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na msiba
huo wa kuondokewa na mmoja wa wanachama na wabunge wake.
Mwenyezi
Mungu awapatie moyo wa subira wakati huu wa majonzi mazito ya kuondokewa na
mpendwa wao, Dkt. Mgimwa.