Uongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB),
umesema Yanga itake isitake AzamTV itarusha mechi zote na kama hawataki
ni bora wakajitoa kwenye Ligi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya
Ligi, Ahmad Yahaya akijibu azimio lililofikiwa na viongozi na wanachama
wa Yanga wa kugomea AzamTV kuonyesha mechi zake.
Yahaya alisema Yanga hawana haki ya Televisheni za Ligi Kuu mwenye haki hizo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
“Haki za Televisheni za Yanga wanazo wenyewe wala
sisi hatujawaingilia, wanauamuzi wao kama watauza haki hizo kwenye mechi
zao za kirafiki, mechi za kimataifa hilo ni jukumu lao wala sisi
halituhusu.
“Lakini haki za Ligi Kuu ni za TFF, Ligi Kuu ni
mali ya TFF ambayo Bodi inasimamia, na Yanga itaheshimu misingi, kanuni,
na maelekezo yote yanayotolewa na TFF, Azam imeingia mkataba na TFF
kupitia Bodi ya Ligi ambao ndio wasimamizi, Yanga hawana haki yoyote ya
kukataa mechi zao zisionyeshwe na AzamTV.
“Wao Yanga kama hawataki AzamTV iwatangaze basi
ijitoe kwenye ligi sisi hatutawatangaza, lakini madhali wapo kwenye ligi
basi mechi zao zitaonyeshwa na huo ni msimamo wa Bodi na Serikali,”
alisisitiza
Yahaya alisema kuwa fedha za Yanga Sh75 milioni
ambazo wamezisusa bado zipo kwenye akaunti ya Ligi Kuu na iwapo muda
wowote wakiziitaji watapatiwa fedha hizo.
Kauli ya Yahaya imekuja siku chache baada ya Yanga
kuzungumzia suala la mkataba wa AzamTV kwenye mkutano wao mkuu na
wanachama kuwataka viongozi wao kuwapeleka mahakamani Azam kwa kukiuka
agizo la Yanga la kutaa mechi zao za Ligi kuonyeshwa live na kampuni
hiyo.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusufu Manji alitoa
mchanganuo wa udhamini huo kwa kusema “Azam wanataka kuonyesha mechi
zetu kwa Sh100 milioni, kwa mechi 26 tunazocheza ligi nzima hiyo ni sawa
na Sh3 milioni kwa kila mechi, kwa mechi yetu moja tunapata zaidi ya
Sh3 milioni na ile inayotukutanisha na Simba tunaingiza zaidi ya Sh100
milioni na kuhoji wanachama wake udhamini huo ni halali au siyo halali
ambapo kwa pamoja waliukataa kwa kile walichoeleza siyo halali na kutaka
Azam wapelekwe mahakamani.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo,
Clement Sanga akizungumzia suala hilo mara baada ya mkutano huo alisema,
“Kuna kampuni ambayo tumeingia nayo mkataba SGM ya Kenya kwa ajili ya
kuonyesha mechi yetu ya raundi ya kwanza dhidi ya Al Ahly ya Misri,
kampuni hii kwa mechi moja tu inatupa Dola 55,000 (sawa na Sh90
milioni).
“Tulikubaliana na Azam TV wao wabaki na kipindi
cha Yanga Soccer Show, sisi tuendelee na Haki zetu za Televisheni na
Zuku, lakini yaliyotokea hapa katikati yanajulikana,” alisema.
“Wanachama wameamua tuwapeleke mahakamani AzamTV,
lakini sisi kama viongozi tutakaa na uongozi mpya wa TFF, na wanasheria
wetu kuangalia upya suala hili, milango bado ipo wazi kwa Azam kukaa
meza moja na sisi.”alisema Sanga.