Naitwa Cyril August Chami (PhD) Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini na Mjumbe wa NEC-CCM kupitia Wilaya ya Moshi Vijijini.
Nimesikitishwa
na kufadhaishwa sana na mtu au watu waliotengeneza akaunti kwa jina
langu kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook na kujifanya yeye au wao
ndio mimi.
Wamepachika
hata picha zangu zinazopatikana kirahisi kwa sababu ya majukumu ambayo
nimeshawahi kuwa nayo kama Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, na Waziri wa
Viwanda na Biashara.
Hilo lenyewe, yaani kutengeneza akaunti kwenye Facebook kwa jina la mtu na kuweka picha zake bila ridhaa yake, ni kosa la jinai.
Lakini
ubaya zaidi ni kwamba mtu huyo au watu hao wanawasiliana na wapiga kura
wangu kule Moshi Vijijini na walio nje ya jimbo na kuwauliza kero
zinazowakabili. Wanawajibu hao wananchi kana kwamba wao ndio mimi. Kwa
vile wao sio mimi, majibu yao siyo sahihi. Lakini kwao hilo halina
tatizo maana nia yao ni kunichafua.
Wanaenda
mbali zaidi na kukitukana Chama changu cha Mapinduzi wakionyesha kuwa
mimi ni shabiki na/au sympathiser wa CHADEMA. Wanatukana wanachama
wenzangu wa CCM na kwa maana hiyo, viongozi wangu wa CCM.
Naamini
wanajua kuwa nia yao hii ni ovu lakini nawaomba watambue kuwa
hawatafanikiwa katika malengo yao kwa sababu mtetezi wangu ni mkubwa
kuliko nia hiyo yao.
Siyo
siri kuwa asilimia kubwa ya mawasiliano kwenye mitandao yanafanyika kwa
anwani feki, hivyo wajue kuwa hata wasomaji wangenishangaa sana kama
ningejiundia akaunti ya Facebook, niweke picha zangu, halafu NIANZE
KUWATUKANA VIONGOZI, WANACHAMA NA CHAMA CHANGU CHA MAPINDUZI.
Ifahamike
kuwa wakati wao wanawauliza wananchi wangu kero zao kwa Facebook wakiwa
kwenye viyoyozi mimi nilikuwa naongea na wananchi hao ANA KWA ANA, siyo
tu kuzijua kero zao bali kuzitatua.
Kwa
mfano, kuanzia December 20 hadi Januari 17 nimetembelea Kata za Uru
Kusini, Uru Kaskazini, Mbokomu, Old Moshi Mashariki, Old Moshi
Magharibi, Kimochi, Kibosho Kati, Okaoni, Kibosho Magharibi, Kibosho
Mashariki, Mwika Kaskazini na Mwika Kusini. Nimefika pia TPC
kumuonyesha DED wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi sehemu ya kujenga
daraja la Samanga litakalounganisha vijiji vya Mikocheni na Chemichemi
kwa shs 250 millioni na pia tumetembelea Kata ya Uru Mashariki kukagua
barabara inayoanzia Kishumundu Parish hadi Materuni, na ambayo tuko
mbioni kui-grade kwa shs 700 milioni na harakati za kuipata hiyo fedha
zinakwenda vizuri.
Nimeshiriki
fundraising ya kujenga ukumbi wa kisasa Mawella Parish Kata ya Uru
Kusini, fundraising ya kujenga bwalo Mangi Meli Sekondari Kata ya Old
Moshi Mashariki na fundraising ya kuvijengea uwezo vikundi 16 vya WEKEZA
kata za Okaoni na Kibosho Kati. Kabla ya hapo nilishiriki fundraising
ya kujenga jengo la utawala Uru Seminari katikati ya Novemba 2013.
Ningekuwa
mtumiaji wa Facebook ningepost events hizi zote na hata kutaja kiasi
tulichopata na kiasi cha michango yangu na rafiki zangu.
Hilo sikufanya.
Kwa nini?
Ni kwa
sababu asilimia 98 ya wananchi hawa niliowatembelea hawatumii Facebook,
nalijua hilo, ndiyo maana nawatembelea kituo kwa kituo nikitambua
nikiwasiliana nao kwa Facebook nitapata majibu kutoka kwa asilimia 2 ya
wapiga kura, tena walio nje ya jimbo. Na katika kipindi chote hicho
sikuweza kwenda kwenye mitandao kwa sababu nilikuwa vijijini kwenye
ziara kama Katibu Mwenezi wa CCM Moshi Vijijini, Ndugu Hussein Jamal
alivyopost siku chache zilizopita.
Watambue
kuwa rekodi yangu ndani ya Bunge, CCM na Serikali inafahamika kuwa mimi
si mpayukaji, sina ushabiki na upinzani, na ni kati ya makada
wanaoipenda CCM kwa vitendo zaidi kuliko maneno. Kwa maana hiyo wengi wa
wasomaji waliosoma hayo wanayonipandikizia wameshaanza kutia shaka kama
huyo ndiye Chami wanayemfahamu, na katika hili wako sahihi.
Watambue
pia kuwa kama nia yao ni kuniharibia ndani ya CCM na jamii
wameshashindwa kwa sababu maneno ya kupandikiziwa kwa wiki moja hayawezi
kuaminika zaidi ya rekodi yangu inayofahamika tangu Uru Seminari
nilikokuwa Mwenyekiti wa UVCCM kwa miaka 3, Chuo Kikuu cha Dar
nilikokuwa Rais wa Wanafunzi Kampasi ya Mlimani, Ikulu nilikokuwa
msaidizi wa Rais masuala ya Uchumi, Mbunge, Naibu Waziri na Waziri.
Bila
shaka wote nilioishi nao katika maeneo haya na kwingineko watakiri kuwa
mimi si mwepesi wa kujisifu, kupayuka na wala si mtu wa matusi kwa mtu
binafsi, viongozi wa dini, wa Chama au wale wa Serikali.
Wakati
nawaonya waache siasa hizi chafu, nawatahadharisha pia kuwa za mwizi ni
arobaini! Ipo siku mtu huyu au watu hawa wataumbuliwa na jamii.
Dr Cyril August Chami.
Mbunge wa Moshi Vijijini.