Ticker

6/recent/ticker-posts

MUSTAFA AKONAY AONGOZA MATEMBEZI YA HISANI

Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mkoani Manyara, Mustafa Akonaay ameongoza matembezi ya hisani kwa kuwatembelea wagonjwa wa hospitali ya wilaya hiyo na kuwagawia vyakula, sabuni na nguo kwa lengo la kuwafariji.

Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo juzi kwa wagonjwa wa hospitali hiyo, Akonaay alitoa wito kwa jamii kuwajali wagonjwa, kwani nao wanatamani kusherehekea sikukuu wakiwa majumbani mwao wao na familia zao.

“Jamii iige mfano kwa kujali wagonjwa na kupitia siku hii ya Boaxing day na mimi natoa msaada huu kidogo niliojaliwa ili nanyi mjisikie kuwa tunawajali na kuwathamini japokuwa mpo hospitalini mkipata matibabu,” alisema Akonaay.

Alisema wagonjwa ni watu wanaohitaji upendo, faraja na kutiwa moyo kwani wenyewe hawakupenda kuwa katika hali hiyo, hasa kwa wakati huu wa mwisho wa mwaka ambao familia nyingi zinakutana kwenye sherehe mbalimbali.

Kwa upande wao, baadhi ya wagonjwa waliokuwa wanapatiwa matibabu kwenye hospitali hiyo ya wilaya ya Mbulu, walimshukuru mbunge huyo kwa kuwajali kwa kuwatembelea, kuwafariji na kuwapa zawadi za sikukuu.

“Mimi namuuguza mtoto wangu hapa hospitalini ila namshukuru mheshimiwa Akonaay, kwa kutufariji na kutupatia zawadi wakati huu wa kumalizia sikukuu ya krismas na kuukaribisha mwaka mpya wa 2014,” alisema Martha Bura.

Naye, Joyce Ombay ambaye ni mkazi wa kata ya Uhuru mjini Mbulu alisema wamefarijika baada ya kutembelewa na mbunge huyo wakiwa hospitalini na kuiomba jamii iige mfano huo kwa kuwapa kipaumbele wagonjwa na maskini.

Post a Comment

0 Comments