Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema halijaupokea vizuri uteuzi wa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Juma Nkamia kwani linamuona kama ni mpinzani wa tasnia ya habari nchini. Hata hivyo, MCT limesema halimwingilii Rais Jakaya Kikwete kwa maamuzi yake kwani huwateua anaowaona wanafaa kwa sababu ni wasaidizi wake kulingana na malengo aliyonayo.
Akizungumza na NIPASHE jana Mwenyekiti wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema uteuzi wake umelisikitisha baraza hilo kwani Nkamia ni mtu asiye na nia njema na vyombo vya habari kulingana na matamshi yake bungeni na kwingineko.
“Tunatambua kazi ya uteuzi ni ya rais na hatumwingilii katika hili, lakini sisi kwa uteuzi wa Nkamia tunaona kama ni meseji ambayo Rais anatutumia ambayo si nzuri sana kumteua mtu asiye na nia njema na vyombo vya habari kuwa katika wizara hii,” alisema Mukajanga.
Alisema ni ngumu kufanya kazi na Nkamia kwa sababu ya msimamo wake wa
kupinga uhuru wa vyombo vya habari na pia uelewa wake kuhusu dhana ya
vyombo vya habari kujisimamia vyenyewe na dhana ya utangazaji kwa ajili
ya umma.
Mukajanga aliongeza kuwa MCT itaendelea kufanya kazi na
serikali. Lakini alisema pia kuwa baraza litaendelea kuhimiza
upatikanaji na usimamizi wa sera na sheria za vyombo vya habari. Naye
George Mbara, mkazi wa Dodoma alisema ameshangazwa na uteuzi wa Nkamia.
“Siku zote bungeni Nkamia hakuwahi kutetea vyombo vya habari na siku
zote amekuwa akiponda waandishi wa habari, Jukwaa la Wahariri na MCT
akiziita kuwa ni taasisi ambazo hazina faida...leo hii ataongozaje
taasisi ambazo amekuwa akizidharau?” alihoji.