Vituo sita vya
afya vilivyopo Wilaya ya Babati na Hanang’ Mkoani Manyara, ambavyo vilikuwa
vinatoa huduma ya afya vijijini bila nishati ya umeme tangu vianzishwe, vitafungiwa
nishati hiyo ili viondokane na tatizo hilo.
Akizungumza na
waandishi wa habari juzi mjini, Mkurugenzi wa kampuni ya Lucas-EMS, Mhandishi
Samwel Kessy alisema kampuni yake imejiandaa ipasavo kuhakikisha vituo hivyo vya
afya vinanufaika ipasavyo na nishati hiyo.
Mhandisi Kessy
alitaja vituo hivyo vya afya ambavyo vimeshafungiwa nishati hiyo ya umeme hafi
hivi sasa ni Qameyu na Secheda vilivyopo wilayani Babati na kituo cha afya cha Bassodesh
kilichopo wilayani Hanang.
Alisema katika
mpango huo wanatarajia kufunga nishati ya umeme wa jua na upepo ambapo hivi
sasa vituo hivyo vitatu vimeshanufaika na huduma hiyo na vituo vya Gidas cha
Babati, Dumbeta na Getanuwas vya Hanang’ vitafuata.
“Mfumo huo wa
umeme ambao unatumia nguvu ya upepo na mionzi ya jua kwa pamoja, utafanya kazi
kwenye jokofu la kuhifadhi dawa, taa, kompyuta, kipimo cha damu, radio, runinga,
X ray na vinginevyo,” alisema Mhandisi Kessy.
Nao, baadhi ya wauguzi
wa vituo hivyo vya afya, Paulina Tsaxara, Adelina Munishi na Juliana Nyalolo,
wamepongeza hatua hiyo ya kuwekewa umeme kwani awali walikuwa wanatoa huduma
kwa jamii katika mazingira magumu.
Walisema hivi
sasa huduma zao zitakuwa makini baada ya kufungiwa nishati hiyo ya umeme ambayo
awali ilikuwa vigumu kufanya shughuli zozote zinazohitaji umeme hivyo kuwakwamisha
kwa kiasi kikubwa.