Kutokana na mgogoro mkubwa wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji unaoendelea wilayani Kiteto ambao umefikia hatua ya kusababisha maafa makubwa ya umwagikaji wa damu, mauaji ya watu na uharibifu wa mali, Wizara Kivuli, Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa umma;
Tunatambua kuwa baada ya maafa hayo makubwa kuwa yametokea tayari, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitakiwa kufanya ziara katika eneo hilo jana ambayo hata hivyo haikufanyika na sasa imeelezwa kuwa atakwenda leo, kutafuta suluhu ya mgogoro huo ambao ni moja ya vielelezo vya Serikali ya CCM ambayo yeye ni mtendaji mkuu, namna ambavyo imeshindwa kuweka sera bora ya ardhi na kuwajibika ipasavyo kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji;
Tunamtaka Waziri Mkuu Pinda atakapokwenda Kiteto kujionea kwa macho athari za mgogoro huo ambao umedumu kabla na baada ya mwaka 2006, achukue hatua za kinidhamu kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Martha Umbulla na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Jane Mutagurwa, kisha amshauri Rais Jakaya Kikwete awafute kazi wote wawili mara moja.
Waziri Mkuu anapaswa kumshauri rais amfukuze kazi DC Umbulla kwa sababu akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kiteto, amezembea kuwajibika ipasavyo na kusababisha kukosekana kwa usalama wa raia na mali zao katika eneo hilo, hadi kutokea kwa umwagikaji wa damu na mauaji makubwa.
Halikadhalika, Waziri Mkuu Pinda pia achukue hatua za kinidhamu na kumshauri Rais Kikwete amfukuze kazi Mkurugenzi wa Wilaya Jane Mutagurwa, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa halmashauri, kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo kuweka mipango bora ya mgawanyo wa ardhi kwa matumizi mbalimbali kwa wananchi wa eneo husika, hali ambayo ingeweza kuepusha maafa hayo.
Kwa ujumla viongozi hao wa wilaya wameshindwa kutumia nafasi zao kutoa utumishi bora kwa umma ambao ungesaidia kutatua mgogoro huo na kuepusha hali inayoendelea sasa. Hata Mkuu wa Mkoa wa Manyara amenukuliwa kwenye vyombo vya habari akikiri mbele ya mkutano wa hadhara, kwamba mgogoro huo unakuzwa na uongozi huo.
Aidha, tunataka taarifa zote zilizopo kuhusu mgogoro huo wa ardhi Kiteto ambao umekuwepo kabla na baada ya 2006, ziwekwe hadharani ili umma utake uwajibikaji wa viongozi wengine ambao kwa namna moja pamoja na kujua chanzo cha mgogoro kwa muda mrefu, walishindwa kuchukua hatua mapema hali ambayo ingesaidia kuliepusha taifa na aibu hii ya wananchi wake kupigania na kuuana kwa ajili ya ardhi, badala ya kuishi na kufanya shughuli zao kama ndugu, kwa ajili ya familia zao, jamii na taifa kwa ujumla.
Kupitia nafasi ya Waziri Kivuli katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), baada ya kupata taarifa za kina za mgogoro huu, nitaitaarifu na kuishauri Kambi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ili ichukue hatua za kibunge na pia Chama kichukue hatua nje ya bunge katika suala hili kipekee na tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji kwa ujumla wake, katika maeneo mengine nchini.
Imetolewa leo Januari 16, 2014 na;
David Silinde (MB)
Waziri Kivuli, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI).
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia