Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Liberatus Sabas akiongea na askari, viongozi wa vyama na serikali,
vikundi vya ulinzi shirikishi pamoja na wananchi wa eneo la Tarafa ya
Themi wakati wa kuwatambulisha askari 15 watakaoungana na wananchi wa
eneo hilo katika utendaji wa kazi za kipolisi za kila siku.(Picha na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Viongozi
wa serikali za mitaa,Askari, vikundi vya ulinzi pamoja na wananchi
wakimsikiliza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas wakati akielezea mikakati ya
Polisi 15 watakaokuwa wanafanya kazi katika tarafa ya Themi pamoja na
wananchi wa eneo hilo.
Jumla
ya askari 45 ambao walikuwa wanafanyakazi Kituo Kikuu cha Polisi Arusha
na Kitengo cha Usalama Barabarani wametawanywa katika tarafa tatu za
jijini hapa. Askari hao kutoka vitengo mbalimbali wamesambazwa katika
tarafa za Themi, Elerai na Suye wakiwa ndani ya kikosikazi ambacho
kinajumuisha askari wa Upelelezi, Usalama barabarani na askari wa
kawaida ambapo lengo kubwa ni kushirikiana kwa ukaribu na wananchi.
Akizungumza
na wananchi katika matukio ya ukaguzi wa tarafa hizo pamoja na
kuwatambulisha askari hao jana tarehe 10.01.2014 katika tarafa hizo,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP) Liberatus Sabas amesema kwamba, jamii katika maeneo yao ikiamua
kupinga uhalifu toka ngazi ya familia kwa kushirikiana na nguvu ya
askari hao hakika uhalifu utapungua kama si kutokuwepo kabisa.
“Hapo
awali jeshi la Polisi lilikuwa na askari kata lakini baadae likawa na
askari tarafa na kuona kwamba hiyo haitoshi sasa limeamua kuanzisha
kanda za kitarafa ambapo kila tarafa itakuwa na askari 15 kutoka vitengo
mbalimbali watakaoongozwa na Mkaguzi wa Polisi, hali hii itasaidia
kujenga ukaribu kati ya wananchi na jeshi la Polisi na kutatua matatizo
mbalimbali ya kiusalama kabla hata ya kufika ngazi ya wilaya”.
Alifafanua Kamanda Sabas.
Kamanda
Sabas aliendelea kusisitiza kwa kuwaomba viongozi wa tarafa hizo
kuhakikisha kwamba, vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo vimeundwa
viendelee kuwa hai ili ustawi wa usalama wa watu na mali zao uendelee
kuwepo. Pia aliwaomba waendelee kukusanya michango toka kwa wananchi wa
maeneo yao ili zisaidie kuwapa posho askari wa vikundi vya ulinzi
shirikishi na kununulia vitendea kazi kwani jukumu la ulinzi ni
watanzania wote na hasa wazalendo na kila mmoja aone umuhimu wa amani na
usalama.
Alisema
pamoja na wananchi hao kujitahidi kupambana na uhalifu na kuwakamata
wahalifu lakini baadhi yao huwa hawajitokezi kutoa ushahidi mahakamani
hali ambayo inasababisha watuhumiwa waachiwe huru na kupata ujasiri
hivyo kuweza kujiunga na makundi mengine kuendelea kufanya uhalifu.
Kamanda
Sabas alitoa namba zake tatu za simu kwa wananchi hao ili ziweze
kusaidia katika mawasiliano na kuongeza kwamba, japo kuwa askari hao 15
wapo katika maeneo yao, bado wapo huru kuwasiliana naye na viongozi
wengine katika kupeana taarifa za uhalifu na wahalifu huku akisisitiza
pia ofisi yake ipo wazi kwa wale watakaotaka kwenda kumuona.
Kwa
upande wake Diwani wa Tarafa ya Themi kutoka kata ya Unga Limited
Mh.Issa Omari (CCM) alisema kwamba mpango huo wa askari 15 kupelekwa
katika tarafa hiyo utasaidia katika kudhibiti vitendo vya uhalifu kwani
kutakuwa na nguvu ya pamoja ya ulinzi ambayo itakuwa inajumuisha askari
wa Jeshi la Polisi na vikundi vya ulinzi shirikishi.
Diwani
huyo wa Unga Ltd aliwataka askari wa vikundi vya ulinzi shirikishi
wasirudi nyuma bali wanatakiwa kusonga mbele na yeye pamoja na wananchi
wanaliunga mkono Jeshi la Polisi kwa mpango huo; huku akiongeza kwa
kusema kwamba katika kata yake uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa baada
ya kuwepo kwa ushirikiano kati ya jeshi la Polisi, viongozi wa mtaa huo
na vikundi vya ulinzi shirikishi.
Naye
Diwani wa kata ya Elerai Mh. Mhandisi Jeremiah Mpinga wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tarafa ya Elerai alisema, sasa umefika
wakati wananchi wa eneo lake waondoe itikadi zao za vyama badala yake
wote washirikiane katika suala zima la kuimarisha ulinzi huku akiwata
viongozi wa mitaa kuhamasisha uanzishaji zaidi wa vikundi vya ulinzi
shirikishi ili washirikiane na askari wa jeshi la Polisi huku akiunga
mkono mpango huo kwa kauli mbiu yake isemayo “ULINZI KWANZA MAISHA
SALAMA”.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia