RAIS Jakaya
Kikwete ameshauriwa katika mchakato wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
kumtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kujieleza
kwake na umma ili kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa dhidi yake
kutokana na ongezeko la bei ya umeme.
Kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Waziri Kivuli wa Nishati
na Madini, John Mnyika (CHADEMA), Rais Kikwete anapaswa kutambua kuwa
Waziri Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013
alipowahakikishia wananchi kuwa bei ya umeme haitapanda hata baada ya
Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha
bei ya nishati hiyo.
Alisema
kinyume na kauli za Prof. Muhongo, Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), katika kikao cha Desemba
10, mwaka jana, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango
mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja, hatua ambayo itaongeza
mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.
Wakati
Mnyika akisema hayo, wananchi wamependekeza kwamba iwapo mamlaka husika
hazitapunguza kiwango cha ongezeko la bei ya umeme; maandamano
yaandaliwe kuishinikiza serikali kuchukua hatua za haraka za kunusuru
uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na ongezeko hilo.
Mnyika
ambaye ni mbunge wa Ubungo, alisema kuwa uamuzi wa kupandisha nishati
hiyo ulifikiwa Oktoba 11, mwaka jana, baada ya TANESCO kuwasilisha
maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Ewura, iliyopendekeza kuongeza
bei kwa asilimia 67.87 kuanzia Oktoba 1, mwaka jana, asilimia 12.74
kuanzia Januari 1, mwaka huu na asilimia 9.17 kuanzia Januari 1, mwaka
2015.
“Vilevile
TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme
kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumko wa bei na mabadiliko ya
thamani ya shilingi ya Kitanzania hatua ambazo nazo zina athari katika
uchumi na maisha ya wananchi,” alisema.
Kuhusu
wananchi kuandamana, alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo aliomba
kufikishiwa maoni ya wadau katika kipindi cha wiki moja juu ya athari za
ongezeko hilo na hatua ambazo wananchi wanapendekeza zichukuliwe
kurekebisha hali hiyo.
“Kabla ya
kipindi hicho kumalizika tayari nimepokea maoni ya wananchi kutoka
katika mikoa mbalimbali nchini. Hakuna mwananchi yeyote mpaka hivi sasa
kati ya waliotuma maoni kwa njia ya barua pepe aliyeunga mkono ongezeko
hilo la bei ya umeme,” alisema.
Mbunge huyo
alisema kuwa wananchi hao wameelezea athari ambazo wameanza kuzipata
huku wakipendekeza hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa kunusuru uchumi wa
nchi na ongezeko la gharama za maisha linalotokana na ongezeko la bei
ya umeme.
Alisema kuwa
wananchi wamependekeza kwamba badala ya mamlaka kukimbilia kupandisha
bei ya umeme ni muhimu kuchukua hatua za kupunguza mzigo mkubwa wa
gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na
uendeshaji wa sekta ya nishati.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia