Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanzia leo,
kinarusha helkopta tatu kwa siku 14 mfululizo, katika kutekeleza
kampeni iliyopewa jina la Operesheni Pamoja Daima (ODB) itakayoendeshwa
katika mikoa yote nchini.
Ziara hiyo inaanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza
na Ruvuma, huku viongozi wa chama hicho wakijigawa katika makundi sita;
matatu yakitumia helkopta na matatu yatawafikia wananchi kwa kutumia
usafiri wa magari.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema jana
jijini Dar es Salaam kuwa, lengo la operesheni hiyo ni kukiimarisha
chama hicho na kuwafumbua macho wananchi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
“Viongozi wakuu wa chama, wabunge, wenyeviti wa
mikoa, wilaya, majimbo na kanda kila mmoja atashiriki kwa nafasi yake
katika operesheni hii. Tutafanya mikutano kwa wiki mbili, ila tunaweza
kuongeza wiki nyingine moja.”
“Naomba tueleweke, katika hili hatufanyi kampeni
hata kidogo, huu ni mwendelezo wa maandalizi ya chaguzi mbalimbali. Kama
mnakumbuka tulianza kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya
kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kwa sasa tunachokifanya ni kuongeza nguvu na
umakini zaidi. Makundi yataanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na
Ruvuma, tutapita kila Kata ambazo utafanyika uchaguzi wa madiwani.”
Mbowe alisema operesheni hiyo itapiga kambi katika
Jimbo la Kalenga ambalo kwa sasa lipo wazi baada ya mbunge wake ambaye
pia alikuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa kufariki dunia
Januari 1, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haijatangaza
kufanyika uchaguzi katika CHAjimbo hilo, Chadema tutafika Kalenga na
tutafanya mkutano maalumu na kutoa pole kwa wakazi wa jimbo hilo
kutokana na msiba mkubwa wa mbunge wao,” alisema Mbowe.
Operesheni hiyo inafanyika siku chache tangu chama
hicho kikuu cha upinzani nchini kipite katika mgogoro ambao
ulisababisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kukimbilia
mahakamani ili kunusuru uanachama wake.
Wakati Zitto akinusurika kufukuzwa kutokana na
zuio la mahakama, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson
Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo walifukuzwa
uanachama, likiwa ni hitimisho la mchakato ulioanza kwa kuwavua nyadhifa
zao pamoja na Zitto.