HOFU
ya harakati za Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kuwania urais katika
uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani imezidi kukitesa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), safari hii Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), ukitaka
atimuliwe.
Jana UVCCM imemtaka Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula,
kuwang’oa watu wanaotangaza kuwania uongozi kabla ya wakati, na
wanaomwaga fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu ili kuwashawishi wawaunge
mkono katika nia zao.
Tamko hilo la UVCCM linakazia kauli iliyotolewa wiki iliyopita na
Mangula, kuwa CCM itawaadhibu makada wake wanaotangaza au kufanya
kampeni za urais kabla ya wakati uliowekwa na chama hicho.
Wakati chama hicho kikionekana kutikiswa na ushawishi wa Lowassa,
mbunge huyo anadaiwa kuendelea kujiimarisha katika kile alichokiita
safari ya kuwapatia Watanzania elimu bure kwa kukutana na
wafanyabiashara wa mkoani Arusha.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa Januari 2, mwaka huu,
Lowassa aliendelea na harakati zake za kujipanga kugombea urais 2015 kwa
kuwaandalia chakula cha mchana marafiki zake zaidi ya 100.
Hafla hiyo ilifanyika majira ya saa saba mchana kwenye eneo la Papa
King lililopo karibu na hoteli ya Lush Garden ambalo hutumika kwa
michezo ya watoto.
Kwenye hafla hiyo, Lowassa hakutoa hotuba, badala yake alikuwa
anapita kwenye meza za wageni wake na kuwashukuru kwa kuhudhuria ibada
yake ya shukurani aliyoifanya siku ya mwaka mpya.Kwa mujibu wa mmoja wa watu walioshiriki kwenye hafla hiyo, mbunge
huyo alikuwa akiwaomba wasisite kuitikia wito wake wa kukutana nao Juni
1, mwaka huu.
Alibainisha kuwa mkutano huo wa Juni 1 utawakutanisha marafiki,
wanasiasa na wafanyabiashara mbalimbali, na watachangisha fedha za
kutekeleza mikakati yake ya kuifikia safari aliyoianza mwaka huu.
Katika kikao kilichofanyika Januari 2, mwaka huu, kada wa CCM
aliyekuwa mbunge katika Mkoa wa Mwanza mwaka 2005-2010, alikabidhiwa
jukumu la kuratibu posho na fedha za kujikimu kwa baadhi ya watu
waliohudhuria.
UVCCM wataka atimuliwe
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu
Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi Taifa, Paul Makonda, alisema Kamati
ya Maadili inayoongozwa na Mangula, inapaswa itafasiri hasira ya wanaCCM
kwa vitendo.
Makonda alisema UVCCM wameamua kuwa wakali kwa watu wasiofuata kanuni
na ilani ya chama chao, ambacho kinaweza kuanguka kama kisipowadhibiti.
Ingawa katika mkutano wa jana Makonda hakutaja majina ya makada wa
CCM wanaodaiwa kukiuka kanuni kwa kutangaza nia mapema, lakini
anaonekana kumlenga Lowassa.
Licha ya kuonekana kumlenga Lowassa, si Mangula wala Makonda
waliokuwa na ubavu wa kutaja hadharani jina la mbunge huyo aliyetangaza
safari ya kuwaletea Watanzania elimu bure na huduma bora za kijamii.
Lowassa katika hotuba yake ya kufunga mwaka 2013 na kuukaribisha
mwaka mpya 2014 nyumbani kwake Monduli, alikaririwa akisema ameanza
rasmi safari aliyoiita ya matumani ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza
ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya
uhakika.
Mbunge huyo ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi
ya urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu wa 2015, aliyasema hayo katika
ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli.
Katika hafla hiyo, Lowassa anadaiwa kuwasafirisha baadhi ya wajumbe
wa vikao muhimu vya uamuzi vya chama na kuwapa fedha, malazi na kadi za
Krismasi ambazo zinadaiwa kuambatanishwa na fedha.
Kauli ya UVCCM, kumuonya Lowassa na wengine wanaodaiwa kuvunja
kanuni, inafanana na ile ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na
ya Mangula, ambaye alikaririwa hivi karibuni kuelezea kuundwa kwa timu
ya kuwachunguza makada wake wanaodaiwa kutangaza nia ya kuwania uongozi
kabla ya wakati.
Kwa upande wa Nape, yeye alikaririwa akidai kuwa Lowassa amevunja
kanuni, hivyo kupoteza sifa ya kugombea nafasi za uongozi ndani na nje
ya CCM.
Makonda alisema kuwa vijana wa CCM hawatakubali kuona mshikamano
unavunjika kwa sababu ya watu wanaogawa fedha na kuahidi kutoa elimu
bora.“Watu wanatangaza kutoa elimu bora kwanini wasifanye hayo kupitia
chama, kinachofanywa sasa ni mwelekeo wa kubomoa mshikamano ndani ya
CCM, kudhoofisha na hatimaye kutuengua katika uongozi wa nchi,” alisema.
Makonda alisema watu hao ni wasaliti wasio na woga wala aibu kwa
kujiaminisha kuwa wanagombea urais, ubunge, udiwani na nafasi nyingine
za kupigiwa kura baada ya kuanza kampeni za kishindo za rushwa na
vishawishi mbalimbali nje ya utaratibu, kanuni na maadili ya CCM.
“Hali hii inatishia kabisa kutoweka kwa mshikamano ndani ya chama, na
inasababisha makundi yanayoundwa na wagombea hawa wasio rasmi
yanayopita nchi nzima kushawishi kwa fedha na rushwa nyingine kwa
makundi ya kijamii, ya kijasiriamali ili kuungwa mkono.
“Watu hawa wameweka pembeni ilani ya CCM ya 2010 na kutumia ilani zao
binafsi za kumwaga pesa nchi nzima, kusambaza elimu kama njugu bila
kuelezea vyanzo vya mapato vya serikali zao za kusadikika,” alisema.
Alisema kuwa CCM ina taratibu za kupata uongozi, hivyo kufanya
kinyume ni uasi, upungufu wa busara na ukosefu wa sifa ya uongozi hali
inayozidi kukitia doa chama.“Dhamira ya CCM ni kutuunganisha wote kuwa kitu kimoja, dalili zozote
nje ya tunu hizo ni usaliti, hauna budi kupigwa vita kwa nguvu zote,
hasa sisi vijana, na tusiangalie nyani usoni kwani hakuna mtu yeyote
aliye juu au mkubwa kuliko chama, hivyo bandu bandu hii iliyoanza
tusiivumilie itatuweka pabaya,” alisema Makonda.
Alisema kuwa asiyetaka kufuata maadili, miiko na kanuni za CCM ni ruksa kuondoka.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia