Leticia Ghati na Haji Ambar Khamis jana
wamechaguliwa kuwa Makamu Wenyeviti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, katika
Mkutano Mkuu wa Nane wa chama hicho uliofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond
Jubilee.
Ghati ambaye amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti
(Bara) alikuwa akiwania nafasi hiyo na Anyimike Mwasakalali, Rakia
Abubakar Hassan na Danda Juju ambao walijitoa kugombea dakika za mwisho.
Kwa upande wa Ambar Khamis(Makamu Mwenyekiti Bara) alipita bila kupingwa kutokana na kuwania peke yake nafasi hiyo.
Msimamizi wa Uchaguzi huo, Moses Machali ambaye
pia ni Mbunge wa Kasulu Mjini, aliwatangazia wajumbe wa mkutano huo kuwa
Ghati na Ambar ni wagombea waliokosa upinzani, bila kufafanua sababu za
wapinzani wa Ghati kujitoa.
Awali katika ufunguzi wa Mkutano huo, Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alikitahadharisha Chama
Cha Mapinduzi (CCM), kuacha mpango wake wa kutaka kukwamisha Mfumo wa
Muungano wa Serikali tatu uliopendekezwa katika Rasimu ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Pia CCM kimetakiwa kutambua ya kuwa siku
kitakapoondoka madarakani viongozi na wanachama wake wataendelea kuwa
katika hali ya usalama na wala hakuna atakayelipiza visasi kwa kushindwa
kusimamia umwagikaji wa damu za Watanzania wasiokuwa na hatia.
Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa vyama vya
upizani waliohudhuria mkutano huo alisema: “Serikali tatu siyo sera ya
chama chao sisemi kwamba ni lazima wakubali serikali mbili au nne au
moja sisemi hivyo, ila kauli kwamba siyo sera yao ni kiashirio kwamba
wanaangalia masilahi ya chama na si ya Taifa,” alisema Mbowe huku
akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.
Akitoa salamu za CCM, Mangula alisema hakuhudhuria
mkutano huo kwa lengo la kujibu mapigo, bali kuangalia jinsi uchaguzi
huo utakavyokuwa na mmoja wa wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD).
Awali Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
alisema damu za Watanzania zinazomwagika ardhini bila hatia zinatokana
na utawala mbovu wa CCM.
“Tunataka maridhiano ya kitaifa, tuzungumze,
turidhiane pamoja kwa kuweka masilahi ya Taifa na rasilimali kwanza
vyama badaye.” aliongeza
Naye Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi aliwataka wajumbe wa mkutano huo kutumia fursa hiyo kuwachagua
viongozi watakaokuwa na taswira ya kuwafikisha mbali katika siasa.
“Wanachama hii ndiyo nafasi pekee ya kuwachagua
viongozi bora ambao wamekomaa na wastaarabu watakaowaepusha na migogoro
na wenye sura ya utaifa,” alisema Jaji Mutungi