Mamia ya washiriki tayari
wanajiandikisha kwa wingi kupitia mtandao wa intaneti ili kushiriki mbio za
Kilimanjaro Marathon 2014 zinazotarajiwa kufanyika Moshi tarehe 2 Machi, 2014.
John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa
Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo amesema katika taarifa yake kwa vyombo
vya habari jana kwamba idadi kubwa ya washiriki wanaendelea kujiandikisha
kupitia tovuti yam bio hizo www.kilimanjaromarathon.com
ukilinganisha na mwaka jana ambapo wachache walijiandikisha kupitia mtandao.
Uandikishwaji huo wa mtandao ambao upo wazi mpaka tarehe 18 Februari, 2014
unawapa urahisi wa kujiandikisha hasa washiriki kutoka nje ya nchi ambao
wanatakiwa kujiandaa na safari ya kuja nchini kutokana na mtandao huo kutoa
uthibitisho wa usajili mara tu baada ya kujaza taarifa husika.
Addison aliongeza kuwa ongezeko
kubwa la usajili kupitia mtandao ni ishara kwamba mbio za mwaka huu zitakuwa na
washiriki wengi zaidi wa kigeni ukilinganisha na zaidi ya 400 walioshiriki
mwaka jana. “Ongezeko la ushiriki lina maana kwamba mbio inazidi kukua kwa
kiasi kikubwa na hii ni kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na Kilimanjaro
Premium Lager ambao wamewekeza kwenye mbio hizi tangu zilipoanzishwa mwaka 2003.”
Pia Addison alisema ukuaji wa mbio
hizi ni matokeo ya jitihada kubwa zinazofanywa na waandaaji kupitia mtandao wa
intaneti pamoja na mbio hizi kuonyeshwa bara zima la Afrika kupitia SuperSport
na televisheni nyingine za kimataifa dunia nzima.
Zikiwa zimepangwa kufanyika Moshi
tarehe 2 Machi, 2014, mbio za Kilimanjaro Marathon zitakuwa na matukio manne
ambayo mbio ndefu za 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon, 21km Nusu Marathon, 11km GAPCO Disabled Run (zitahusisha
viti vya magurudumu na baisikeli za mikono tu), na mbio za kujifurahisha za Vodacom
5km Fun Run ambazo hutoa fursa kwa watu wa rika zote kushiriki.
Kwa mara nyingine tena mbio hizi
zitakuwa kivutio kutokana na ushiriki wa timu zitakazowakilisha makampuni
mbalimbali kupitia shindano la Half Marathon Corporate Challenge.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia