Wakulima wa zao
la ufuta wa Tarafa ya Mbugwe, Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, wametakiwa
kujiunga na mpango wa stakabadhi ghalani ili kunufaika kiuchumi kuliko kunyonywa
na walanguzi.
Wito huo
ulitolewa na Ofisa masoko wa shirika la Farm Africa, Rahel Pazzia wakati wa mafunzo
ya kuwajengea uwezo wakulima wa zao la ufuta, yaliyofanyika juzi kwenye kijiji
cha Mwada wilayani Babati.
Pazzia alisema
kati ya wakulima 920 wa zao hilo katika eneo la Mbugwe, ni wakulima 135 pekee
waliojiunga na mfumo wa stakabadhi ghalani na wakiulizwa kwanini hawajiungi na
mfumo hawana jibu sahihi la kutoa.
“Mfumo wa
stakabadhi ghalani unafaida kwa mkulima kwani unatumia bidhaa zilizohifadhiwa kama
dhamana, badala ya mali na kuliko kuweka nyumba au kiwanja rehani ili kupata
mkopo na wengi wamekopeshwa,” alisema Pazzia.
Naye, Ofisa
ushirika wa halmashauri ya mji wa Babati, William Mbogoro, akizungumza kwa
niaba ya bodi ya leseni za maghala nchini alisema wadau wa mfumo huo ni mweka
mali, mtunza ghala, asasai za fedha, taasisi za Serikali na mnunuzi.
Mbogoro alisema mfumo
wa stakabadhi ghalani una manufaa kwa wakulima kwani uwezo wao wa kuhifadhi
mazao ni mdogo na hawafahamu namna bora ya kuyapanga hivyo kusababisha
kupunguza ubora wake.
Nao baadhi ya
wakulima hao wa ufuta, Haji Daudi, Katarina Madolo, Mwajuma Lubuva na Philemon
Lissu, walidai kuwa watajiunga na mfumo huo kwani awali walikuwa hawajatambua
umuhimu wake.
Walisema kupitia dhana
ya stakabadhi ghalani watayaweka mazao yao sehemu husika na kuwa dhamana ya kupatiwa
mikopo kwenye taasisi za fedha kuliko kuweka nyumba, kiwanja au gari hivyo
kufilisiwa pindi ukishindwa kurudisha.