TAASISI ya Utafiti wa Dawa za Mimea na Wadudu (TPRI) yenye makao
makuu mkoani Arusha imekumbwa na kashfa ya ubadhirifu wa fedha zaidi ya
sh milioni 317 ambazo hazijulikani matumizi yake mpaka sasa.
Kutokana na tuhuma hiyo, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) imetuma tume ya watu watano kufanya ukaguzi wa
ubadhirifu wa fedha hizo zinazodaiwa kuwa na utata wa matumizi yake.
Tume hiyo inayoongozwa na Edmund Gratian inatokana na maagizo
yaliyotolewa kwa ofisi hiyo ya CAG na Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC) chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, baada
ya kubainika kuwepo kwa wasiwasi wa ubadhirifu huo.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, wasiwasi huo ulitokana na kiasi hicho cha
fedha kutolewa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwenda kwa TPRI
kwa ajili ya kutekeleza tafiti mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo
na kisha kurejeshwa wizarani bila kuandikiwa ripoti wala maelezo
yoyote.
Mbali na ubadhirifu huo, tume hiyo inachunguza pia kuwepo kwa
mazingira tata ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Epiphania
Kimaro, kwa kuwa yaligubikwa na mizengwe na mazingira ya rushwa na
hayakufuata mfumo sahihi.
Zitto alisema kabla ya uteuzi huo Bodi ya TPRI iliteua majina matatu
ya watumishi waliokuwa na sifa ya kushika nafasi hiyo na kuwasilisha
wizarani, lakini cha kushangaza baadaye aliteuliwa mtu tofauti kushika
nafasi hiyo, tena asiye na sifa na kuahidi kuwa kamati yake itafuatilia
kujua sababu za maoni ya bodi kutofuatwa katika uteuzi huo.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wafanyakazi wa taasisi
hiyo walisema wamefurahishwa na hatua ya serikali kuleta tume hiyo
kufanya uchunguzi, kwakuwa itabaini mengine mengi.
Walisema Machi mwaka jana wafanyakazi saba wakiwamo wanne wa Idara ya
Uhasibu na watatu wa idara nyingine walifukuzwa kazi kutokana na
ubadhirifu wa zaidi ya sh milioni 360 wa fedha za mishahara.