Bingwa
wa ngumi wa uzito wa kilo 68 wa Mkoa wa Manyara, Ramadhan Songe kutoka wilaya
ya Simanjiro, ametetea ubingwa wake kwa kumpiga bondia wa Mji mdogo wa
Mirerani, Swaleh Masudi.
Songe
alishinda pambano hilo la raundi 10 juzi Kazamoyo Inn, lililoandaliwa na
Kampuni ya Ken Family, kupitia Nick Electronics, Pub and Barber shop ya Mji
mdogo wa Mirerani, chini ya Mkurugenzi wake Kilonzo Kalaghe.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Meneja wa Ken Family, Ally Kayoyo alisema Songe alishinda
pambano hilo lililosimamiwa na Mwenyekiti wa CCM wa kata ya Endiamtu Issa
Katuga, kwa kupata alama 50 kwa 20.
“Kupitia
Mkurugenzi wetu Kilonzo Kalaghe tumeamua kudhamini ngumi na tutaendelea kuleta
mapambano mengine kwa ajili ya kunyanyua michezo katika maeneo ya mji mdogo wa
Mirerani na Manyara kwa jumla,” alisema Kayoyo.
Hata
hivyo, akizungumza baada ya kumalizika pambano hilo na kutangazwa mshindi,
Songe alisema anastaafu kucheza ngumi kwani hivi sasa hana mpinzani kwenye mkoa
huo, hivyo anatumia muda wake kwa kuwafunda vijana chipukizi.
“Kwa
vile ngumi zipo kwenye damu yangu nitawafundisha vijana wenye nia ya kujifunza
ndondi, ili kuuendeleza mchezo huu ambao nimetumia nguvu zangu nyingi kwa ajili
ya kuunyanyua katika mkoa wa Manyara,” alisema Songe.