Naibu
Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana akishuka katika kazi za mahakama
ya kazi, Tume ya Usuluhishi na Upatanishi wiki iliyopita siku ya Jumanne jijini
Dar es Salaam.
Bi
Itika kasambala akiwa katika picha tofauti jijini Dar es Salaam baada ya kuelezea
sakata lake na Naibu Waziri wa kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.
Na. Mwandishi wetu
NAIBU Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dkt
Makongoro Mahanga ameingia kwenye kashfa nzito ya kuvunja sheria za kazi nchini
kwa kumfanyisha kazi msaidizi wake (PS) wa ofisi yake Bunge kwa miaka kumi bila
mkataba na kumlipa fedha taslimu shilingi laki mbili tu (200,000) kama mafao.
Naibu Waziri, Mahanga anakuwa kiongozi wa kwanza kuingia
kwenye kashfa akiwa madarakani tena kwenye swala la ajira wakati yeye mwenyewe
ni waziri mwenye dhamana na maswala ya ajira na haki za wafanyakazi nchini
chanzo chetu kimeelezwa.
Kwa mujibu wa sheria kazi na mahusiano kazini, Naibu Waziri
amekiuka kifungu cha 3 cha sheria ya Taasisi za kazi za mwaka 2004 na pia
amekiuka sehemu ya tatu ya viwango vya ajira na sehemu ndogo A kwa kushidwa
kuandika mkataba kwa mujibu wa kifungu cha 14 ibara ya kwanza kama sheria ya
kazi na mahusiano kazini inavyotaka.
Katika kifungu hicho cha 14 ibara ya kwanza kinasema mkataba
utakuwa wa kipindi cha muda usiotajwa, mkataba wa kazi maalumu na mkataba
unatakiwa kuwa wa maandishi ambapo vyote Mhe Naibu Waziri hakufanya.
Ibara ya 15 kifungu cha.-(1) kinasema kwa kuzingatia
masharti ya kifungu kidogo cha (2) cha kifungu cha 19, mwajiri anatakiwa kumpa
mfanyakazi, wakati mfanyakazi anapoanza kazi, taarifa zifuatazo kwa maandishi,
jina, umri, anuani ya kudumu na jinsia ya mfanyakazi; mahali alipoajiriwa; kazi
zake; tarehe ya kuanza; muundo na muda wa mkataba; kituo cha kazi; masaa ya
kazi; ujira na njia ya ukokotoaji wake, na taarifa za mafao mengine.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni jijini
Dar es Salaam, Bi. Itika Kasambala (31) anasema alianza kazi kwa Mbunge huyo wa
Segerea na Naibu Waziri wa kazi Dkt. Mahanga, mwaka 2003 kama PS (Personal
Secretary) kwa makubaliano ya kumpa mshahara wa shilingi 120,000 kwa mwezi
lakini alianza kumlipa shilingi 50,000 tu.
“aliniambia kwamba
nianze kazi kwanza baadaye atanipa mkataba wa ajira na kunilipa mafao ya
hifadhi ya jamii na matibabu lakini baada ya miaka kumi ananitumia sms akiwa
Dodoma kwamba kazi basi sikuhitaji tena,” Kasambala alisema.
Amesema kwamba Mbunge huyo alimtumia sms akiwa kwenye vikao
vya bunge mjini dodoma mwaka jana mwezi wa sita akimjulisha kwamba ajira yake
imeshafika kikomo kwa sababu hana uwezo tena wa kumlipa mshahara na mahitaji
mengine ya kiofisi.
Kasambala aliendelea kusema kwamba mara ya kwanza wakati
anaanza kazi mwezi wa tano mwaka 2003 baada ya msaidizi wa ofisi ya mbunge
Mahanga kuacha kazi na ndipo alipotafutwa yeye na walikwenda kuelewana kwa
malipo ya 120,000 kwa mwezi.
Alisisitiza kwamba mara baada ya kuanza kazi kwa ofisi ya
mbunge alikuwa analipa pesa kupitia mkononi na baadaye tigo pesa na baada ya
muda akawa anachukua pesa yake ya mshahara toka katika manisapaa ya Ilala kama
posho ya Mhe Mahanga kama diwani kila mwezi.
Dada huyo kwa mshangao baada ya mahojiano ya muda mrefu
alikiri kwamba Mhe Mahanga alikuwa na nia ya dhati kuanzisha mahusiano ya
kimapenzi na kumtaka aende Dodoma lakini alikataa kufanya masharti hayo.
“mwaka juzi baada ya kuonyesha nia ya kunitaka kimapenzi
alinipigia simu akitaka niende Dodoma bungeni kwa mazungumzo zaidi kama
msaidizi wake lakini nilikataa,’ aliongeza Kasambala.
Amesema tangu aanze kazi kwa Mhe Mahanga hakuwa anatoa
huduma zozote kama matibabu au fedha kwa ajili ya sikukuu ilikuwa ni mshahara
tu wa 120,000 kwa mwezi lakini kila akimfuata ili waandikishiane mkataba
alikuwa akizungumsha bila sababu za msingi.
Bi. Kasambala aliongeza kuwa amefanya kazi Mhe Mahanga tangu
akiwa mbunge wa Ukonga na baadaye Segerea lakini ameshidwa kuheshimu sheria za
ajira na taratibu za kazi wakati yeye mwenyewe ni waziri mwenye dhamana ya
ajira kwa watanzania.
Amesema mwaka jana tarehe 14/09/2013 alimtumia kwa Tigopesa
kiasi cha shilingi za Tanzania 200,000 kama mafao yake baada ya kufanya kazi
kwa takribani miaka 10 kama Msaidizi wake wa Ofisi ya Mbunge.
Amesema kwamba aliamua kwenda Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi,
Mahoteli, Majumbani na Kazi Nyingine (CHODAWU) kwa msaada wa ksiheria ba baada
ya kukutanishwa bado Mhe Mahanga akawa mgumu kukubaliana kiungwana mpaka
ikawalazimu kwenda mahakani Tume ya Usuluhishi na Upatanishi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi wakili wa Kasambala,
Nyaisa Godwin alisema kuwa kesi imefunguliwa mahakama ya kazi wiki iliyopita
siku ya Jumanne, Tume ya Usuluhishi na Upatanishi kesi namba
CMA/DSM/ILA/R.711/13.
Wakili Nyaisa alisisitiza kwamba Naibu Waziri aliiambia
mahakama kwamba Dada Kasambala alikuja kufanya kazi kwake kama mwanafunzi wa
chuo kwenye mazoezi lakini alishidwa kuithibitishia mahakama kwa ushawishi wa
barua ya (field to chuoni).
“tulishagazwa na majibu ya waziri kwamba dada huyo alikuwa
field, na nilimuuliza field ya miaka kumi? Alishidwa kutoa jibu mbele ya
mpatanishi (Arbitrator),” amesema Nyaisa.
Nyaisa aliendelea kusema kutokana na matatizo ya kuachishwa
kazi ghafla bila taratibu dada huyo amepata maradhi ya presha, vidondo vya
tumbo na maradhi mengine baada ya kufanya kazi kwa Mhe Mbunge kwa miaka kumi
bila matibabu wala kulipiwa mifuko ya hifadhi za jamii.
Wakili Nyaisa aliongeza kwamba kesi hiyo ya aina yake dhidi
ya Naibu Waziri wa Kazi itasomwa tena tarehe 13/02/2014 katika Tume ya
Usuluhisho na Upatanishi.
Juhudi za kumtafuta, Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na
Maendeleo ya Vijana, Dkt. Mahanga hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya
kiganjani kushidwa kupatikana kwa muda mrefu alipotafutwa kwa ajili ya kutoa
ufafanuzi.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia