Huenda mpango wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kufanya vizuri katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ukatibuliwa kufuatia tishio lililopo la chama kipya cha siasa cha ACT.
Duru za siasa zinakitazama Chama cha ACT chini ya
Zitto Kabwe aliyefukuzwa Chadema hivi karibuni, kama tishio kubwa kwa
upinzani nchini. Ni chama kinachoweza kusababisha CCM iendelee kuwa
kinara katika chaguzi za Tanzania.
Zitto, mwanasiasa machachari aliyejiunga na ACT,
anatajwa kujijengea ngome katika baadhi ya maeneo yanayotegemewa na
Ukawa, jambo linaloelezwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa
kuwa huenda likazorotesha nguvu ya upinzani, endapo chama hicho
kichanga katika siasa kitaamua kusimamisha wagombea katika maeneo hayo.
Baadhi ya mikoa inayoonekana kuwa tegemeo kwa
upinzani chini ya Ukawa na ambayo Zitto anaonekana kujenga himaya yake,
ni pamoja na mkoa wa Kigoma wenye zaidi ya majimbo sita ya uchaguzi
ambayo yanategemewa na upinzani.
Mikoa mingine ni Mtwara, Lindi, Shinyanga, Kagera, Katavi, na Sumbawanga.
Kwa Kigoma majimbo yanayotajwa kuwa hatarini
kumezwa na ACT yanatajwa kuwa ni pamoja na Kigoma Mjini, Kigoma
Kaskazini, Kigoma Kusini, Muhambwe, Kasulu Vijijini na Kasulu Mjini.
Majimbo mengine ambayo ACT inaonekana kuwa na
ushawishi na inaweza au kuyatwaa au kusababisha Ukawa kukosa ushindi ni
pamoja na Mpanda na Sumbawanga Mjini.
Zitto ajigamba
Katika kudhihirisha amejipanga vyema kushiriki
Uchaguzi Mkuu ujao na kufanya vyema kupitia ACT ambacho kwa muda mrefu
amekuwa akihusishwa kukiasisi, Zitto anasema:
“Mimi ni mchapakazi, siangalii nyuma tena,
naangalia mbele. Mapambano yanaanza, matokeo mtayaona baada ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka huu.”
Alitoa majigambo hayo alipotangaza kujiunga rasmi
na chama hicho mwishoni mwa wiki, huku akiwa na kundi la watu waliowahi
kuwa wanachama na viongozi wa Chadema.
Swali kuu ni; je, ACT kikiwa katika hatua za uchanga, kinaweza kuleta ushindani katika uchaguzi?