Wabunge wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) jana walianzisha tafrani bungeni na kusababisha kikao cha Bunge
kuvunjika saa 5.18 asubuhi baada ya kusimama na kupaza sauti
wakishinikiza Serikali itoe kauli juu ya hatima ya uboreshaji wa Daftari
la Kudumu la Wapigakura na upigaji wa Kura ya Maoni kupitisha Katiba
Inayopendekezwa.
Huku wakiwa wamesimama walikuwa wanapiga kelele
wakisema, ‘hatutaki kuburuzwa’, ‘tumechoka kupelekeshwa’, Watanzania
wapo njia panda’ na ‘tunataka majibu,’ ‘Bunge lisitumiwe kuilinda
Serikali’, ‘Waziri Mkuu yupo bungeni kwa nini asitoe kauli’ na maneno
mengine mengi bila mpangilio.
Wabunge hao wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na
CUF, kwa umoja wao walimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa majibu
hayo muda huohuo, kabla ya jioni kutoa hutuba na kuahirisha mkutano huo
wa 19 wa Bunge.
Baadaye jana usiku katika hotuba yake ya
kuahirisha Bunge hadi Mei 12, utakapoanza Mkutano wa 20, Waziri Mkuu
Pinda alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itatoa taarifa siku za
hivi karibuni kuhusu upigaji wa kura ya maoni.
“Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha ratiba kamili,” alisema.
Sakata lilivyoanza
Kelele hizo zilitokana na hoja za wabunge wawili,
Suleiman Jafo wa Kisarawe na yule wa Ubungo, John Mnyika waliotaka Bunge
lisitishe shughuli zake zote lijadili suala hilo kwa kuwa ni muhimu na
Taifa halielewi hatima yake, wakati Bunge lilikuwa linaahirishwa jana.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alikataa suala hilo
kujadiliwa, akisema ni hoja iliyowasilishwa katika mkutano uliopita,
akataka Bunge liendelee na shughuli zake, lakini wabunge wa upinzani
walikataa kukaa na wakaendelea kupaza sauti.
Hata alipobadili kauli akasema, “nimesema kauli
itatolewa, wabunge hao walisisitiza itolewe papohapo. Hata alipowataka
waondoke ndani ya ukumbi huo, wabunge hao ambao ni wachache
ukilinganisha na wale wa CCM, walikataa, wakisema; “hatutoki hadi kauli
itolewe.”
Kelele za wabunge hao zilimfanya Spika Makinda
kutoa kauli kali, “Njooni mwendeshe (kikao) nyinyi basi. Njooni hapa
mkae tena wote.”
Baada ya kuona kelele hizo zimedumu kwa dakika
tatu, Spika Makinda alilazimika kusitisha shughuli za Bunge hadi baadaye
(jioni), bila kutaja muda ambao Bunge lingerejea na kuwaacha wabunge
wakiwa wamesimama katika makundi ndani ya ukumbi wakijadili tukio hilo.
Jafo ndiye aliyeanza kuomba mwongozo wa Spika
akitaka chombo hicho cha kutunga sheria kisitishe kujadili jambo lolote
lile, badala yake kijadili mustakabali wa Katiba Mpya, akitaka Serikali
iwasilishe muswada wa sheria kwenye mkutano wa 20 wa Bunge (wa Bajeti)
ili Katiba ya Mpito ipitishwe.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia