Waziri wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza na aliyewahi
kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha, Joshua Kileo (Kulia) baada ya ibada katika kanisa
la KKKT Mjini Kati siku ya Jumapili.
************
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema
pamoja na mitihani mikubwa ambayo taifa inakabiliana nayo, umoja wa
Watanzania utaifanya nchi isonge mbele kama taifa linalozingatia sheria
na demokrasia.
Akizungumza baada ya Ibada ya Jumapili ya Pili ya Pasaka
iliyofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa
Mjini Kati jana, Nyalandu alisema nchi itafanikiwa kupita mitihani hiyo
kama wananchi wataimarisha umoja kati yao.
“Nchi inapita huku kukiwa na mambo mengi makubwa
kufanya…kila mmoja anahitaji amani na hiyo tunaweza kuipata au
kufanikiwa kupita salama iwapo tutakuwa na umoja.
“Nchi yetu itasimama, itashinda mitihani ambayo tunayo kama
ya uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu, upigaji wa
kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba mwaka huu,” alisema.
Mapema katika mahubiri yake kanisani, Mteolojia Solomoni
Dereva, aliwaomba Watanzania kuliombea taifa kwa Mungu ili liweze kupita
kwa utulivu katika kipindi hiki chenye mambo makubwa.
“Tumuombe Mungu pia atuletee viongozi wazuri, wenye sifa
ambao watatutoa hapa tulipo na kutufikisha mbele zaidi katika
maendeleo,” alisema.
Alisema kiongozi mzuri ni sawa na mchungaji mwema ambaye
huanza kuchunga nafsi yake dhidi ya matendo maovu kama rushwa na
ubinafsi na pia huchunga familia yake na ofisi aliyokabidhiwa ili
kuwatumikia wananchi.