Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza askofu Mpya wa Jimbo Katoliki
Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu wakati wa ibada ya kumweka wakfu
iliyofanyika katika kanisa kuu la Parokia ya Mama mwenye Huruma,
Ngokolo, mjini Shinyanga jana.
---------------------------------
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Aprili
12, 2015 ameungana na maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Shinyanga,
kuhudhuria Ibada rasmi ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu mpya wa Jimbo hilo,
Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu.
Rais Kikwete
aliwasili jana kwenye Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga kiasi
cha saa sita unusu mchana kwa ajili ya Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na
maaskofu wakuu, maaskofu na maaskofu wasaidizi 38, akiwamo Askofu Mkuu wa Jimbo
la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Rais wa Mabaraza ya
Kipapa na Katibu Mwambata wa Uenezaji Injili Ulimwenguni Askofu Mkuu Protase
Rugambwa kutoka Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican.
Askofu Sangu ambaye
amewekwa wakfu na kusimikwa kwenye Siku ya Huruma ya Mungu Duniani anakuwa
Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga na anachukua nafasi iliyoachwa wazi tokea
Novemba 6, 2012, wakati aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo, Baba Askofu Aloysius
Balina alipofariki dunia.
Kwa miaka karibu
mitatu, jimbo hilo limekuwa chini ya Usimamizi wa Kitume wa Askofu Mkuu Yuda
Tadei R’uaichii wa Jimbo Kuu la Mwanza.
Askofu Sangu mwenye
umri wa miaka 52 baada ya kuwa amezaliwa Februari 19, mwaka 1963, katika Kijiji
cha Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, alipata daraja la
upadrisho Julai 3, mwaka 1994. Wakati anateuliwa na Baba Mtakatifu Francesco
kuwa Askofu Februari 2, mwaka huu wa 2015, alikuwa na daraja la Mosinyori.
Akikabidhi
Jimbo hilo kwa Askofu mpya, Askofu Mkuu R’uaichii amesema kuwa Jimbo la
Shinyanga ni moja ya majimbo makubwa zaidi ya Kanisa Katoliki nchini, likiwa na
kilomita za mraba karibu 30,000 na waumini Wakatoliki wanaokaridiwa kufikia
300,000 katika Mkoa ambao idadi kiasi ya wakazi wake bado wanaamini imani za jadi.
Amesema kuwa Jimbo
hilo lina parokia 29, mapadre wa Jimbo 52, mapadre wa Kitawa 18 na hivyo
kulifanya jimbo hilo kuwa na jumla ya mapadre 70 na “jeshi kubwa” la watawa 70.
Kwenye sherehe hizo
zilizohudhuriwa na viongozi wengi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Mheshimiwa Ali Lufunga, Askofu Sangu amepewa zawadi ya sh milioni
18, fimbo ya kiuchungaji na ng’ombe 10 wa maziwa na Wakatoliki wa Jimbo hilo.
Rais Kikwete amerejea Dar es Salaam jioni ya leo baada ya kumalizika kwa Ibada hiyo.