Baadhi ya mashamba ya migomba yaliyofyekwa na kijiji kwa madai kuwa shamba hilo lipo ndani ya eneo la kijiji,
Baadhi ya wahanga waliovunjiwa nyumba zao wakiwa katika mabaki ya nyumba hizo ,katika kijiji cha Sakila wilayani Arumeru
FAMILIA saba zenye watu zaidi ya 30 katika kijiji cha
Sakila,wilayani Arumeru mkoani hapa,hazina mahala pa kuishi kutokana na nyumba zao kubomolewa na
mwenyekiti wa kijiji hicho kwa madai kuwa zilijengwa bila kufuata utaratibu.
Aidha familia hizo wakiwemo watoto wadogo zimelazimika kulala
kwenye mabaki ya nyumba hizo licha ya baridi kalli na mvua zinazonyesha
wilayani humo baada ya kukosa mahala pa kujikimu.
Akizungumzia kadhia hiyo mmoja wa wahanga hao,Samson Joseph
Nasary(70) alisikitishwa na hatua ya mwenyekiti wao Richard Mbise akiwa na
kundi la watu zaidi ya 20 kuvamia makazi yao na kubomoa nyumba zao huku
wakimwaga akiba kidogo ya chakula walichokuwa nacho .
Alisema tukio hilo limetokea April 2 mwaka huu ambapo askari
wa kampuni ya ulinzi ya Kifaru ndio walikuwa wakitekeleza zoezi hilo
wakiongozwa na uongozi wa kijiji hicho.
‘’Eneo hilo ni mali ya baba yetu mzee Joseph Mareu Nasary
aliyeishi hapa tangu mwaka 1948 na baada ya kufariki alituachia urithi
tukiwa tunaishi hapa,wakati kijiji kinaanza mwaka 1976 /77 sisi tayari
tunaishi hapa sasa tunasikitika sana leo hii kuvamiwa na kuvunjiwa nyumba zetu
wakisema eti tumevamia’’alisema
Naye mkazi mwingine Peter Mafie alilalamikia hatua ya
mwenyekiti huyo kuamuru kufyekwa kwa
migomba yake na mazao aliyootesha kwenye shamba lake bila kushirikishwa
.
Alieleza kuwa kabla ya kumchagua mwenyekiti wao,aliwahidi
kuwa angewasaidia kutatua mgogoro huo bila kuondolewa kwenye makazi yao,suala
ambalo lilichangia wao kumchagua kwa kishindo.
Hata hivyo wameshangaa baada ya
kumchangua amewageuka na kubomoa nyumba zao.
Wengine waliobomolewa nyumba zao ni,Lightnes Charles ambaye
ni mjane,David Israel,Lucas Akyo ,Visenti Mathias ,Joshua Shayo,Deatres Sakwera
na Selian Juma wote wakazi wa kijiji hicho.
Aidha wameitaka serikali akiwemo mbunge wao Joshua Nasary
kuwasaidia wapate haki yao ya kurejeshewa makazi hayo kwani kwa sasa wanaishi
kwa kubangaiza na kulala mahala pasipo stahili.
Kwa upande wa mwenye kiti,Richard Mbise alikiri kubomoa
nyumba za wakazi hao akisisitiza kuwa alikuwa akitekeleza amri ya mahakama ya
ardhi ya wilaya iliyotoa ushindi kwa kwa uongozi wa kijiji.
Hata hivyo alisisitiza kuwa wananchi hao walivamia eneo
hilo lililotengwa kwa ajili ya huduma
mbalimbali za kijiji ikiwemo ujenzi wa zahanati na shule na kuanzisha makazi.
Aliongeza kuwa uongozi
wa kijiji ulijaribu mara kadhaa kuwaondoa katika eneo hilo lakini walikuwa wakaidi
hadi suala hilo walipoamua kulifikisha mahakamani.
habari na libeneke la kaskazini blog
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia