KARSAN AWASHUKIA VIONGOZI WA DINI, WANAHABARI

IMG_0481
Mgeni rasmi Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues (wa pili kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyanza jijini Mwanza kushiriki maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani duniani ambapo kitaifa yamefanyika jijini Mwanza. Kushoto ni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi na wa pili kulia ni Afisa Mfawidhi Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa Mwanza, Bw. Ludovick Ringia.(Picha na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Na Modewjiblog team
WAKATI viongozi wa dini wametakiwa kuacha kufanya siasa na badala yake wahubiri upendo na si upinde, waandishi wa habari wameelezwa kununuliwa na wanasiasa kulainisha maneno yao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho Siku ya Amani Duniani iliyofanyika Mwanza.
Alisema katika mazungumzo yake hayo kukengeuka kwa wanahabari na viongozi wa dini ambao ni wadau muhimu wa amani hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi ni kasoro inayotakiwa kufutwa mara moja.
Akikazia kwa viongozi wa kidini alisema kwamba amani ya nchi inahitaji kulindwa na wote lakini viongozi wa dini wana wajibu mkubwa katika hilo.
Alisema kutokana na wadhifa wake amekuwa akipata habari nyingi ambazo zinakengeuka na zenye mwelekeo hatarishi na nyingi zinakuwa ni za viongozi wa dini.
“Habari zinapoandikwa Tanzania, inapofika saa saba, saa nane ya usiku, mimi huletewa habari nyingi sana, kuziangalia na miongoni mwa habari tulizozizuia ni mbaya kweli kweli zinatoka kwa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini.” alisema Karsan
IMG_1136
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho Siku ya Amani Duniani iliyofanyika kitaifa jijini Mwanza.
“Sasa nawaomba sana kwa unyenyekevu mkubwa kwa viongozi wa dini nchini, nawaomba muhubiri upendo na msihubiri upinde!..” alisisitiza Karsan.
Kiongozi huyo wa UTPC yenye wanachama zaidi ya elfu nne alisema kwamba anashangaa viongozi hao wa dini kugeuka wanasiasa kwani anaamini kwamba Kwa Msajili wa Vyama hakuna chama cha dini kilichosajiliwa.
Alisema pamoja na kwamba hakuna chama cha siasa cha kidini kusajiliwa anashuhudia anashuhudia baadhi ya viongozi wa dini wakihubiri siasa.
Pamoja na kuhimiza viongozi wa dini wasitoke katika mstari wao wa kuhubiri amani, alisema kuna kasoro kubwa miongoni mwa wanahabari kwa kuwa wengi wao tayari wamenunuliwa.
“Wanahabari wengi baadhi yao wameshanunuliwa hasa kwa habari zao wanazoandika nyingi wanawachagulia wananchi kwa habari zao za kununuliwa. Andikeni habari na sio kuandika hatari.” alisema Karsan.
Na kuongeza kuwa: “Magazeti yanapiga kura, radio inapiga kura, Televisheni inapiga kura, tena inapiga kura sasa wakati siku ya kura ni Oktoba 25. Acheni kabisa michezo hiyo kwani tunawaomba muwe waandishi wa habari na sio waandishi wa hatari…Andikeni habari na sio hatari!!” alisisitiza Karsan.
Kwa kuzingatia miiko ya taaluma ya habari nchini, alipigilia msumari kwa wamiliki wa vyombo vya habari, wanasiasa kuacha kuwahonga waandishi hasa kwa kutumia fedha ili kulainisha habari huku wakionekana kuunadi Uhuru wakati mioyoni mwao hawana utu.
“Nawaomba wananchi wa Tanzania, msiwachague viongozi wa nchi hii kupitia magazeti, radio na Televisheni. Puuzeni habari zote nendeni kwenye mkutano wa wanasiasa na msikilize kila mgombea anasema nini na kila chama kinasema nini hao wanaoandika kwenye magazeti yao ni yao wenyewe na mengi hayana ukweli.” Alisema.
IMG_1161
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan akisisitiza jambo kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani duniani jijini Mwanza.
UTPC ina zaidi ya waandishi wa habari 4600 nchini kote ambapo makao yake makuu yapo Mkoani Mwanza.
Pia aliwawaomba wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuhakikisha wanawalipa mishahara waandishi wao kwani hadi sasa baadhi yao wanahabari wanadai mishahara zaidi ya miezi mitatu.
“Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari, ili waandishi waweze kufanya vizuri, basi walipeni mishahara yao. Wapo ambao hadi leo baadhi yao wanawadai mishahara zaidi ya miezi mitatu” alifafanua Karsan.
Karsan aliwataka wamiliki hao kuacha kusimama majukwaani na kujinadi mambo mazuri wakati wanashindwa hata kuwalipa wafanyakazi wao mishahara mizuri na hapo hapo wanataka waandike habari za haki.
Aidha alikemea tabia ya wamiliki wa vyombo vya habari ya kuwachagulia habari wahariri.
Naye mwakilishi Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafa hiyo aliwataka watanzania katika umoja wao kuhakikisha kwamba amani inaendelea kuwapo nchini ikizingatiwa kwamba taifa hili lilipata uhuru kwa njia ya amani.
Alisema Tanzania tangu zamani imeweka mbele mazungumzo katika kutatua mambo mbalimbali na kusema hatua hiyo ya mazungumzo ni hatua kubwa ya kidekrasia ambayo imefanikisha amani na kusema ni tumaini lake kwamba itaendelea kuwapo.
Naye Naibu kamishina wa Polisi Charles Mkumbo ambaye ni kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza akizungumza katika hafla hiyo aliwataka wananchi kutii sheria bila shuruti na kwamba jeshi la polisi limejipanga kuzuia uhalifu na vitendo vinavyotia hofu kuelekea na siku ya uchaguzi.
Alisema jeshi lake limejipanga vyema pamoja na kutumia weledi na busara kuelekea uchaguzi, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Aliwatahadharisha wananchi umuhimu wa kulinda amani kwani gharama ya kuipoteza na kutaka kuirudisha ni kubwa.
IMG_1421
Pichani ni viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini nchini waliohudhuria maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani Duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini Mwanza.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post