-->
|
Wasanii katika semina kuhusu BIma Ya Afya iliyofanyika BASATA karibuni |
|
Muwezeshaji Catherine kutoka Mfuko wa Taifa wa BIma ya Afya akitoa maada katika semina ya wasanii kuhusu Bima ya Afya |
|
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Paul Makond aliyekuwa mgeni rasmi katika semina ya Bima ya Afya kwa wasanii |
|
Mwenyekiti wa TAMUNET akipokea kadi za kwanza za Bima ya Afya za wanamuziki, katika ofisi za Mfuko wa BIma ya Afya wa Taifa. |
Mwaka
2004, John Kitime ambaye kwa sasa ndie Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanamuziki
Tanzania (Tanzania Musicians Network-TAMUNET) alihudhuria Mkutano Mkuu wa
Shirikisho la Muziki Duniani –International Federation of Musician (FIM).
Katika mkutano huo moja ya maazimio ya mkutano ule ilikuwa kila nchi ihakikishe
inaanzisha utaratibu wa Bima ya Afya kwa wanamuziki wake.
Mara
baada ya kurudi Tanzania, kwa kushirikiana na viongozi wengine wa TAMUNET, Kitime
alianza kufuatilia uwezekano wa kupata huduma ya Bima hiyo kwa wanamuziki. Kwa
bahati mbaya hakukuwa na njia yenye gharama nafuu ya malipo ya BIma hiyo ambayo
mwanamuziki wa kawaida angeweza kuyamudu. Kulikuweko na kampuni ambayo iliweza
kutoa huduma hiyo kwa gharama ya dola 300 kwa mwaka kwa mwanamuziki mmoja.
Kampuni nyingine za Bima zilizotembelewa hazikuonyesha ushirikiano katika jambo
hilo. TAMUNET iliwasiliana pia na mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa katika kipindi
hico mfuko ulikuwa hauna mamlaka ya kuhudumia watu waliokuwa nje ya ajira ya
serikali na mashirika ya umma. TAMUNET iliwasiliana na Mganga Mkuu wa Serikali,
ambaye alishauri TAMUNET kuwasiliana na NGO moja ambayo ilikuwa na makao yake
makuu Sinza, na kweli NGO hiyo ilikubali kuwa ingeweza kutoa huduma ya Bima ya
Afya kwa wanamuziki kwa gharama ya shilingi 3000/- tu kwa mwezi, lakini huduma
hii ilikuwa ni kwa hospitali kadhaa tu jijini Dar es Salaam. Hilo nalo
lilionekana ni bora kuliko kukosa kabisa, lakini muda mfupi baadae NGO hiyo
ilisema haishughuliki tena na huduma hiyo bali imeelekeza nguvu zake kwa watoto
wa mtaani. Hapo ilifuatia miaka kadhaa ambayo hakukuweko na njia yoyote
iliyowezekana ya kupata huduma hiyo. TAMUNET ilijaribu pia kuwasiliana na
mifuko mingine, lakini kila mara iligonga ukuta aidha kwa ahadi ambazo zilikuwa
zikipigwa kalenda bila kutekelezwa.
Mwaka
2015 hatimae ndipo mlango umefunguka, Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa NHIF,
uliitarifu TAMUNET kuwa umeanzishwa mpango wa Bima kwa Kikoa ambao
ungewawezesha wanamuziki nao kupata Bima ya Afya kwa gharama nafuu. TAMUNET
iliuchangamkia mpango huo kwa kuwa imekuwa ajenda ya chama hiki kwa miaka zaidi
ya kumi.
Wanamuziki
wanachama wa TAMUNET tayari wameanza kufaidi huduma ya Bima ya Afya kwa mwaka
mzima, hii ni baada ya kulipia shilingi 76,800/-. Mpango huu utaondoa aibu ya
wanamuziki kuchangiwa fedha za matibabu kila wanapougua, kwani itakuwa busara
kwa wapenzi na washabiki wa muziki kuchangia mwanamuziki wanaempenda apatiwe
Bima ya Afya kuliko kumchangia fedha za matibabu ya muda mfupi. Baadhi ya
wanamuziki ambao tayari wana bima za afya chini ya mpango huu ni Louiza Nyoni,
Abdul Salvador, Rashid pembe, na wengine wengi wamekwisha anza taratibu za
kupata huduma hii.
|
John Kitime akiwa na kadi yake ya BIma ya Afya aliyoipata karibuni |
|
Kadi za Bima ya Afya za wanamuziki mbalimbali |
|
Louiza Nyoni akionyesha kadi yake mpya ya Bima ya Afya |
Ushirikiano wa Mfuko wa Biam ya Afya na TAMUNET unaweka
uwezekano wa mwanamuziki kuanza kuchanga hata fedha kidogokidogo ili kuweza
kufikisha kiasi kinachotakiwa. Wanamuziki wanaweza kupiga simu au kutuma ujumbe
kwenue simu na 0763722557 ili kupata maelezo ya namna ya kujiunga na huduma
hii. Ukiwa mwanamuziki wa Hiphop, taarab, muziki asili, dansi bongofleva,
huduma hii ni kwa ajili yako kumbuka WAJANJA HUJIWEKEA BIMA YA AFYA- NA WEWE NI
MMOJA WA WAJANJA