Sisi, viongozi wa dini pamoja
na taasisi zinazosimamia mchakato wa uchaguzi (NEC, TAKUKURU, Polisi pamoja na Msajili
wa vyama vya siasa) tuliokutana leo
tarehe 17/9/2015, tumepata nafasi ya kujadili kwa kina suala la uhuru,haki na
amani kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika 25/10/2015 na wajibu wa kila mdau
kuhakikisha kuwa uhuru,haki na amani vinalindwa kipindi hiki.Suala la uhuru
haki na amani ni wajibu wetu sisi viongozi wa dini na watanzania wote kwa
ujumla na halina mjadala.Kila mmoja achukuwe nafasi yake kulinda uhuru,haki na
amani na kuweka uzalendo kwanza kuliko kutanguliza maslahi binafsi ya vyama vya
siasa.
Viongozi wa dini wamepata
nafasi ya kujadili na vyombo hivi masuala ya msingi kama kuhakikisha kuwa
maadili ya uchaguzi yanazingatiwa kwa wote, muda wa kutangaza matokeo ya kura
unazingatiwa , haki ya wananchi kupata matokeo haraka ili kuepuka fujo wakati
wa kusubiri na kutangazwa kwa matokeo. Jeshi la polisi kutokutumia nguvu kupita
kiasi, wajibu wa Msajili kuhakikisha vyama vyote vinapata fursa sawa na pia
tumejadili suala la kutumia nyumba za ibada kama sehemu ya jukwaa la siasa.
Viongozi wa dini tumekubaliana
kwa pamoja kuepuka kutumia nyumba za ibada kuonyesha ushabiki wa aina yoyote
kwa chama chochote cha siasa.
Baada ya kujadili kwa kina
masuala hayo viongozi wa dini wanatoa wito ufuatao;
1. Vyombo vya habari vifanye
kazi kwa ueledi bila upendeleo na pia kuhakikisha kuwa inatoa taarifa ya kutosha
kuelimisha umma.
2. Tunaishauri NEC kwenye
chaguzi zijazo iweke utaratibu maalum wa
kuruhusu wanafunzi wa vyuo vikuu waliojiandikisha pamoja na watu wote
waliojiandikisha/watakaojiandikisha waweze kupiga kura.
3. Tunaishauri NEC kwenye
chaguzi zijazo siku ya kupiga kura isiwe
siku ya ibada.
4. NEC iendelee kutoa elimu ya
uraia kuhusu haki ya raia kupiga kura na
haki yao ya kukaa mita mia moja kusubiri
matokeo yatangazwe kwa utulivu kama ambavyo NEC imehakikishia viongozi wa dini
kuwa kila kituo itabandika matokeo yote (Urais,Ubunge na Udiwani)
5. Pamoja na kutimiza wajibu wake wa msingi wa
kulinda raia na mali zao Jeshi la polisi wakati huu wa uchaguzi liendelee kutimiza wajibu wake wa kusimamia
amani na taratibu kwa haki bila upendeleo.
6. Wagombea,wafuasi na wanaowanadi, wanaaswa waache mara moja lugha za
matusi,vitisho,kejeli na kukashifiana vinavyoweza kuchochea fujo na kuleta
uvunjifu wa amani wajikite kunadi sera za vyama vyao.
7.Tunawahimiza wananchi kuwa
makini katika kufuatilia kampeni na sera mbalimbali za wagombea, kuzipima kwa
hali ya juu sera hizo, kutokuuza kadi zao za kupigia kura, kutokununuliwa na
kujitokeza kwa wingi kutumia uhuru na haki yao ya kuchagua viongozi wanao wataka
kwa hiari na amani.
8. Viongozi wa dini wanawahimiza Watanzania
wote kuendelea kuombea nchi hii kuendelea kuwa taifa lililojengwa katika misingi ya uhuru , haki na amani.
9. Viongozi wa dini tutabaki
kuwa manabii na wahubiri wa uhuru,haki na amani wakati huu , wakati wa uchaguzi
na baada ya uchaguzi
Sisi viongozi wa dini Tunawashukuru
Inspekta generali wa polisi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama
vya siasa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kwa ufafanuzi makini na wa kina juu ya
nafasi na utayari wao wa kushirikiana na viongozi wa dini kuhakikisha uhuru,
haki na amani vinaendelea nchini.Maelezo yao na mafafanuzi yao tumeyasikia na tutaendeleza kwa kuwa hiki ni kikao cha mwanzo na tutaendelea kuwa
na vikao vingine pamoja nao kuelekea uchaguzi mkuu ili kufuatilia utekelezaji
na kuendeleza makubaliano yetu katika kuhakikisha uhuru,haki na amani.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia