VUGU VUGU LA AJENDA YA WATOTO NA UCHAGUZI MKUU LAENDELEA KIBAHA MKOANI PWANI.


Mtoto Loida Goodluck Kutoka shule ya Sekondari ya  Simbani akichangia mada katika Mdahalo huo
Mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa mtoto Joyce Michael akizungumza jambo wakati wa Mdahalo  huo
Jastin Moses Mratibu wa mradi wa kuzuia ukatili dhidi ya mtoto kutoka Plan International akichangia mchango wake wakati wa mdahalo huo
 Ombeni Ally Mkuu wa Shule ya Sekondari Simbani akifafanua Jambo katika mdahalo  huo
Ramadhan Lutambi mgombea udiwani kata ya Kibaha maili Moja kupitia Chadema akisisitiza Jambo
 
Rosemary Mkonyi mgombea Ubunge kupitia tiketi ya ACT akizungumza Jambo wakati wa mdahalo huo
Baadhi ya wanafunzi wakiwa wanasikiliza mdahalo huo
Wananchi wakiwa wanafuatilia kwa makini mdahalo huo

Na Mwandishi wetu 
Jamii imetakiwa kuwa karibu zaidi na watoto ili kuhakikisha wanalindwa dhidi ya ukatili na kuhakikisha wanapata haki zao stahiki. Rai hiyo imetolewa na wakazi wa Kibaha Mkoani Pwani katika Mdahalo wa Walinde Watoto uliowaleta pamoja wapiga kura, watoto na wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani.
Kwa upande wake mgombea Ubunge wa Kibaha vijijini kupitia ACT Wazalendo Dk. Rose Mkonyi alisema kuwa chama chake kinaangalia ni kwa namna gani watazingatia katika Lishe bora ya mtoto pamoja na namna gani mtoto atainuliwa Kielimu. Aidha Mgombea Udiwani wa kata ya maili moja kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘CHADEMA’ Ramadhani Lutambi alisema chama chake kitaangalia zaidi afya ya mtoto na kuhakikisha Bohari ya dawa inakuwa na dawa za kutosha.
Hata hivyo, Watoto waliohudhuria mdahalo huo waliwataka wagombea kutimiza ahadi wanazotoa wakati wa Kampeni ili na wao waweze kufikia malengo yao. Watoto walipendekeza serikali ijayo iangalie namna ya kuwalinda hasa wanapoelekea mashuleni kwani wamekuwa wakitembea mwendo mrefu kwenda na kurudi shule ambako wamekuwa wakipata madhara na vishawishi vingi wanapokuwa njiani. 
Aidha watoto pia waligusia suala la rushwa na kwa namna gani linavyorudisha nyuma maendeleo yao na kuwaomba wagombea wa ngazi zote katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa waadilifu ili watoto wapate haki zao.
Mdahalo huo ulioandaliwa na kampuni ya True Vision production chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto wakishirikiana na UNICEF uligusa maeneo kumi muhimu ya uwekezaji kwa watoto ikiwemo kuwekeza kuokoa maisha ya watoto na wanawake, kuwekeza kwenye lishe bora, kuwekeza kwenye usafi, udhibiti wa miundombinu ya maji taka na ugavi wa maji katika shule na kwenye huduma za afya pamoja na kuwekeza katika kumwendeleza mtoto akiwa bado mdogo.
Mengine ni pamoja na kuwekeza kwenye elimu bora kwa watoto wote, kuwekeza katika kuzifanya shule kuwa mahali pa usalama, kuwekeza katika kuwalinda watoto wachanga na wasichana dhidi ya VVU, kuwekeza katika kupunguza mimba za utotoni, kuwekeza katika kuwanusuru watoto na vurugu, udhalilishaji na unyonyaji pamoja na kuwekeza kwa watoto wenye ulemavu. 
Vuguvugu hili la kusambaza ajenda ya watoto kupitia midahalo na wagombea wa nafasi mbalimbali linaendelea kupita mikoa mbalimbali nchini Tanzania kwani tunaamini kuwekeza katika maeneo haya ya kipaumbele kunaweza kupunguza umasikini na kuwezesha kuwepo kwa taifa linalostawi na la usawa.
Unaweza kusikiliza kipindi cha redio cha Walinde Watoto mahali popote kupitia redio shiriki 19 ikiwemo TBC inayorusha matangazo hayo siku ya Jumamosi kuanzia saa nane mchana na pia kupitia tovuti ya www.walindewatoto.org na
 www.facebook.com/WalindeWatoto

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post