SAMIA SULUHU AHAIDI UMEME KILA KIJIJI RUVUMA ,VIWANDA VYA MAHINDI NA KAHAWA


Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Samia Suluhu (katikati) akimnadi mgombea Ubunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Martin Mtonda (kushoto) na mgombea udiwani wa CCM.


MGOMBEA mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Samia Suluhu ameanza ziara yake mkoani Ruvuma akiinadi ilani ya chama hicho huku akiahidi neema kwa wakulima wa kahawa na mahindi wa mkoa huo.

Bi. Samia Suluhu ambaye amehutubia mikutano mitatu katika majimbo mawili ya mkoa wa Ruvuma yaani Jimbo la Nyasa na Mbiga Vijijini, akizungumza katika mikutano yake amesema serikali itakayoundwa na CCM endapo itashinda itahakikisha inashusha umeme katika vijiji vyote vya mkoa huo kwa awamu ili kuchochea maendeleo ya wananchi.

Alisema kwa kuwa mkoa huo unazalisha mazao ya mahindi na kahawa serikali itahakikisha inaanzisha viwanda eneo hilo vya kusaga na kuandaa unga wa mahindi kwa wakulima na kuwawezesha ili wauze unga na kunufaika zaidi tofauti na ilivyo kwa sasa ambapo wamekuwa wakilanguliwa.

Alisema viwanda vingine ambavyo Serikali ya CCM itavianzisha ni pamoja na viwanda vya kubangua kahawa na kuiandaa kikamilifu tayari kwa kutumika, jambo ambalo alisema licha ya kuongeza thamani ya zao hilo itaongeza ajira kwa vijana na kuchochea uchumi wa wakulima eneo hilo.
Akizungumzia miundombinu ya barabara ambayo bado ni changamoto kwa mkoa huo hasa vijijini alisema serikali itakayoundwa na CCM chini ya uongozi wa Dk. John Pombe Magufuli pamoja na yeye watahakikisha wanajenga na kuboresha barabara za maeneo hayo ili ziweze kupitika kwa uhakika.

Hata hivyo kiongozi huyo amesema Serikali itakayoundwa na CCM endapo itashinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015 imejipanga kuboresha vizuri huduma za afya kuondoa ukiritimba na rushwa, elimu kwa kutoa elimu bure toka darasa la kwanza hadi kidato cha nne pamoja na ujenzi wa mabweni na uwezeshaji vijana na akinamama kiuchumi popote walipo mjini na vijijini.

Ziara ya mikutano ya kampeni ya mgombea mwenza huyo wa urais tiketi ya CCM, inaendelea leo katika Mkoa wa Ruvuma na ataingia Jimbo la Tunduru kuendelea kuinadi ilaya ya chama hicho kuomba ridhaa kwa wananchi ili waweze kurejeshwa madarakani na kuunda dola.

Pichani juu ni baadhi ya wananchi na wanaCCM wakiwa wamefurika katika kiwanja cha Kijiji cha Maguu Wilaya ya Mbinga kumsikiliza mgombea mwenza wa urais kupitia tiketi ya CCM alipokuwa akiinadi ilani ya chama hicho.


Pichani juu ni baadhi ya wananchi na wanaCCM wakiwa wamefurika katika kiwanja cha Kijiji cha Maguu Wilaya ya Mbinga kumsikiliza mgombea mwenza wa urais kupitia tiketi ya CCM alipokuwa akiinadi ilani ya chama hicho.
Baadhi ya wananchi na wanaCCM wa Kijiji cha Maguu wilayani Mbinga wakimsubiri mgombea mwenza wa urais, CCM, Bi. Samia Suluhu. 


Pichani juu ni baadhi ya pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda zilizompokea mgombea mwenza wa CCM urais, Bi. Samia Suluhu mara baada ya kuingia Wilaya ya Mbinga zikiwa zimeegeshwa pembeni huku mkutano wa hadhara ukiendelea. 

Mmoja wa wajumbe wa kamati ya kampeni ya mgombea mwenza, Bi. Asumpta Mshama akizungumza na wanaCCM na wananchi (hawapo pichani) katika Kijiji cha Maguu, Wilaya ya Mbinga. 
Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Samia Suluhu (kulia) akizungumza na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, kabla ya kuanza kuhutubia katika mikutano wake wa kampeni.  

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Samia Suluhu (katikati) akizungumza na baadhi ya viongozi wa CCM ambao ni wenyeji wake mkoa wa Ruvuma.

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Samia Suluhu (katikati) akizungumza na mmoja wa vijana walemavu waliohudhuria mkutano wake wa hadhara Kijiji cha Maguu. Bi. Suluhu alimsaidia fedha kijana huyo. 

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post