Taarifa zinazosambaa kumhusu Mkuu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ)
Jenerali Davis Mwamunyange zilizosambaa kwenye mitandao ya jamii
kwamba amekula chakula chenye sumu na amekimbizwa jijini Nairobi nchini
Kenya kwa matibabu hazina ukweli wowote.Ni
uzushi.
Kwa mujibu wa taarifa
za familia ya Jenerali Mwamunyange pamoja na makao makuu ya jeshi ambazo
Globu ya Jamii imezisaka na kuzipata, kiongozi huyu wa JWTZ hivi sasa yupo
nchini Italia kwa ziara ya kikazi ya siku tisa kama anavyoonekana pichani
na hajambo kabisa na yu bukheri wa afya.
Hii ni changamoto kwa wakala wa mawasiliano nchini (TCRA)
ambayo imekuwa ikilaumiwa kwa ukimya wake wa kutochukua hatua thabiti
kuthibiti uongo kama huu kwa kuwatafiti, kuwabaini na kuwachukulia hatua
watu kama hawa wenye nia ya kuleta taharuki na machafuko
nchini.
Wananchi wengie waliohojiwa na Globu ya Jamii
wanahoji endapo kama kweli TCRA ipo na kama ipo ina vifaa vya kisasa
iliyodai wanavyo kuwabaini watu kama hawa, na kwa nini hawajafanya kweli
toka sheria ya mitandao (Cyber Law) iliyoanza
kutumika.
"Endapo kama TCRA watashindwa kumnasa mhusika wa
uongo huu wa kuogofya, inabidi mamlaka husika iangalie upya ajira ya
watendaji wake maana kama taasisi nyeti kama JWTZ inaguswa na wao wakae
kimya tu basi ujue kuna tatizo ambalo inapaswa Serikali ilifanyie kazi",
amesema msomaji mmoja wa Globu ya Jamii katika maoni
yake.