Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa akizungumza na akinamama wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi, UWT (hawapo pichani)Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa akicheza wimbo wa hamasa wa kampeni za CCM kabla ya kuanza kumnadi Dk. Magufuli kwa wanaUWT, Mkoa wa Dodoma. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa akizungumza na akinamama wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi, UWT (hawapo pichani) '...Na wapigwe tu maana hamna namna nyingine..' Mke wa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mama Tunu Pinda akizungumza na akinamama wa UWT Mkoa wa Dodoma.[/caption]
Na Mwandishi Wetu, Dodoma MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa ameweka kando msimamo aliyokuwa nao awali na kuanza kumnadi kwa nguvu mgombea wa nafasi ya Urais kwa tiketi ya CCM, John Pombe Magufuli huku akiahidi atafanya hivyo nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda na shuka hadi shuka. Kimbisa alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma alipokuwa kwenye mkutano na akinamama wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) walipokuwa wakizungumza na mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Bi. Samia Suluhu katika ukumbi wa NEC Makao Makuu ya Chama hicho mjini Dodoma. Tukio la Kimbisa kumnadi mgombea urais wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea mwenza Bi. Suluhu linaonesha tayari kimbisa amefunga ukurasa wa kutokubaliana ambao aliuonesha mapema mjini hapo wakati wa mchakato wa chama hicho kutafuta mgombea mmoja wa urais atakaye peperusha bendera ya CCM. Awali mara baada ya Magufuli kuchaguliwa kupeperusha bendera ya CCM, Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Dodoma, Kimbisa pamoja na wajumbe wenzake wawili, yaani Sophia Simba na Dk. Emmanuel Nchimbi walizungumza na vyombo vya habari mjini Dodoma huku wakionesha kupinga uteuzi huo huku wakidai haukwenda sawia jambo ambalo ni tofauti na sasa. Akizungumza katika mkutano huo aliwataka akinamama wa UWT kuhakikisha wanashirikiana kuhamasisha kampeni za CCM na kutembea nyumba hadi nyumba mtu kwa mtu ili kuinadi ilaya ya Chama Cha Mapinduzi na hatimaye ushindi upatikane. Hata hivyo tayari Dk. Nchimbi naye ameungana na kuanza kumnadi mgombea huyo wa CCM ikiwa ni ishara ya kuvunja makundi. Mapema akizungumza katika mkutano huo, mke wa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mama Tunu Pinda alisema yeye pamoja na mumewe hawawezi kuihama CCM kwa kuwa ndiyo chama pekee chenye sera za kueleweka na zinazotekelezeka ukilinganisha na vyama vingine. Aliwashauri wanachama waliogombea na kushindwa kutokata tamaa na kujaribu kukihama chama hicho kwani asiyekubali kushindwa si mshindani. "...Napendekeza wanao hama vyama wapigwe tu, maana hamna namna nyingine na wapigwe tu, lakini naomba tuwapige kwa kuwanyima kura huko wanapokwenda lakini si vinginevyo," alisema Mama Tunu Pinda alipokuwa akiwasalimu wanachama wa UWT. Katika mkutano huo mgombea mwenza wa CCM, Bi. Suluhu alitaja vipaumbele kwa akinamama endapo watafanikiwa kuunda Serikali, ikiwemo vile vya afya bora kwa mama na mtoto, ujasiliamali kuinua uchumi wa akinamama katika vikundi, uwezeshaji kipembejeo na zana za kisasa kwa akinamama wakulima, na hivyo kuwaomba wanaUWT kumchagua ili aweze kutimiza ndoto za ahadi zake.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com