MILIONI 20 ZAPATIKANA KWENYE ARAMBEE YA MFUKO WA ELIMU NAISINYAI
ZAIDI ya Sh20 milioni zimepatikana
kwenye harambee ya mfuko wa elimu wa kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara wenye lengo la kulipia gharama za masomo kwa wanafunzi wa
sekondari wanaoishi katika mazingira magumu.
Akizungumza kwenye harambee ya
mfuko huo iliyofanyika juzi,Diwani wa kata ya Naisinyai,Klempu Ole Kinoka
alisema mfuko huo ulianzishwa Machi 18
mwaka 2010 na hadi sasa umewezesha kuwasomesha watoto 76 wa kata hiyo.
Ole Kinoka alisema mfuko huo utakuwa
endelevu kwa kuchangiwa kila mwaka na utawanufaisha wanafunzi wa shule za
sekondari za Naisinyai na Ewong’on za kata hiyo wenye uelewa mkubwa darasani
lakini wazazi wao wana hali duni.
Alisema kila mkazi wa kata hiyo
mwenye umri wa miaka 18 kila mwaka anachangia sh10,000 kwa lengo la kutunisha
mfuko huo wenye kusimamiwa na kamati ya maendeleo ya kata baada ya wananchi
kupitia majina ya watoto hao.
“Jamii itaona manufaa na matunda
ya kuchangia mfuko huu baada ya miaka ijayo kwa watoto wetu kwani hili jambo siyo
kama mahindi unapanda leo baada ya miezi kadhaa unavuna faida yake itaonekana
hapo baadaye,” alisema Ole Kinoka.
Naye,Ofisa Mtendaji wa kata ya
Naisinyai,Yeniel Kagonji alisema mfuko huo unakabiliwa na changamoto ya
kuongezeka kwa idadi kubwa ya watoto tegemezi na ukame unaoathiri mifugo na
kilimo kwa wananchi.
Kagonji alitaja changamoto
nyingine ni uelewa mdogo wa baadhi ya jamii juu ya faida ya uchangiaji wa
elimu,wazazi kukabiliwa na michango mingi ya elimu kwa asasi za elimu na
kupanda kwa bei za vifaa na gharama za elimu kuongezeka.
Alisema kutokana na mafanikio ya
kuwasomesha watoto hao 76 jamii nyingi za kata hiyo zimepata moyo na kuhamasika
kuchangia michango mingine ya maendeleo na umewaokoa watoto wengi kupunguza
utoro na kuongeza ufaulu.
Alisema malengo ya kuanzishwa kwa
mfuko huo ni kuunga mkono mchakato wa mpango wa Serikali wa kutekeleza mkakati
wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (Mkukuta) na kuwasaidia watoto
wanaoishi kwenye mazingira magumu.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia