MSAJILI WA ICTR ATEULIWA MSHAURI MAALUM WA MASUALA YA KUZUIA MAUAJI YA KIMBARI
Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amemteua Msajili wa Mahakama ya
Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Adama Dieng, raia wa
Senegal, kuwa Mshauri Maalum wa masuala ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari.
Taarifa
iliyotolewa Jumanne na Idara ya Mawasiliano kwa Umma, ilisema, Dieng
ambaye amekuwa akitumikia nafasi yake ya sasa ICTR tangu mwaka 2001,
anachukua nafasi ya Frances Deng, ambaye Katibu Mkuu huyo anamshukuru
kwa utumishi wake uliotukuka. Deng ambaye ni raia wa Sudan alikuwa
anatumikia katika nafasi hiyo tangu Mei 2007.
‘’Akiwa
mtaalam wa sheria na masuala ya haki za binadamu, Dieng ana utumishi
uliotukuka na mchango wa pekee katika kuimarisha utawala wa sheria,
mapambano dhidi ya kushitaki wahalifu na kujenga uwezo katika nyanja za
mahakama na taasisi za kidemokrasia ikiwa ni pamoja na utafiti,
machapisho na vyombo vya vya habari,’’ taarifa imesema.
‘’Alichangia
pia uanzishwaji wa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali barani
Afrika,’’ taarifa ilifafanua. Dieng alianza kazi kama Msajili wa
Mahakama ya Kanda na Kazi nchini Senegal na kutumikia pia nafasi ya
Msajili wa Mahakama Kuu ya Senegal kwa miaka sita.
Baadaye
Dieng alijiunga na mashirika mbalimbali ya kimataifa akitumikia nafasi
mbalimbali.Alizaliwa Mei 22, 1950 na ni mhitimu wa shahda ya sheria
kutoka Chuo Kikuu cha Dakar.Ametunukiwa vyeti mbalimbali kikiwemo cha
Kituo cha Utafiti katika Chuo cha Sheria za Kimataifa, kilichopo The
Hague, Uholanzi.
Ofisi
ya Mshauri Maalum wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari, ilianzishwa mwaka
2004.Imepewa kazi na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kukusanya
na kutathmini taarifa kuhusu hali ambayo inaweza kusababisha mauaji ya
kimbari kutokea.
Ofisi
hiyo pia ina jukumu la kumshauri katibu Mkuu wa UN, na kupitia kwake,
Baraza la Usalama, kutoa mapendekezo ya kuzuia mauaji ya kimbari.Ofisi
hiyo pia hufanya mawasiliano na mfumo wa UN wa hatua za kuchukua ili
kuzuia mauaji ya kimbari au uhalifu unaohusiana nao.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia