MRITHI WA ICTR AANZA KAZI, LIBYA YAWAACHIA WAFANYAKAZI WANNE WA ICC
Wakati viongozi wa Chombo cha
Umoja wa Mataifa kitakachorithi kazi za Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji
ya Kimbari yaRwandawakiahidi kuwasaka watuhumiwa wakuu wa mauaji
hayo,Libyawiki hii iliwaachia huru wafanyakazi wanne wa Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai waliokuwa wanashikiliwa tangu Juni 7, 2012.
ICTR
Mrithi wa ICTR aanza kazi: Akizungumza katika
uzinduzi wa Chombo cha Umoja wa Mataifa kitakachorithi kazi za ICTR,
Rais wa Chombo hicho, Jaji Theodor Meron Jumatatu wiki hii aliahidi
kuendelea kuwasaka watuhumiwa wakuu wa mauaji ya kimbari yaRwanda ya
mwaka 1994. Kwa upande wake Mwendesha Mashitaka Hassan Bubacar Jallow,
alisema ofisi yake ipo tayari kuanza kushughulikia changamoto kuu ya
Chombo hicho ambayo ni kuwasaka watuhumiwa hao. Watuhumiwa wanaosakwa
vikali ni pamoja na Félicien Kabuga, anayedaiwa kuwa mfadhili mkuu wa
mauaji hayo, Protais Mpiranya, ambaye alikuwa Kamanda wa kikosi cha
walinzi wa Rais na Augustin Bizimana, Waziri wa zamani wa Ulinzi.
Bagosora apelekwa Mali: Mahakama ya
Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari yaRwanda imemhamishia nchini Mali Kanali
Theoneste Bagosora kwenda kutumikia kifungo chake pamoa na wafungwa
wengine watatu. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatano wiki hii,
wafungwa wengine saba wamehamishiwa nchiniBenin kwa madhumunikama hayo.
Awali, Bagosora, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Baraza katika Wizara ya
Ulinzi nchiniRwanda alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya
kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. Hata hivyo,
kifungo hicho kilipunguzwa hadi miaka 35 jela baada ya kukata rufaa.
RWANDA
Wafaransa watua Kigali kufanya uchunguzi:
Ujumbe wa Kifaransa ambao umejikita katika makosa ya uhalifu dhidi ya
binadamu umewasili jijini Kigali Jumatano wiki hii kwa ajili ya kufanya
uchunguzi. Ujumbe huo utakutana na Mwandesha Mashitaka Mkuu pamoja na
wakuu wa kitengo cha kuwasaka watuhumiwa wa mauaji ya kimbari. Kuna kesi
takribani 20 nchini Ufaransa zinazowahusu Wanyarwanda wanaotuhumiwa
kuhusika katika mauaji ya mwaka 1994.
ICC
Libya yawaachia wafanyakazi wa ICC: Mamlaka nchini
Libya Jumatatu wiki hii iliwaachia huru wafanyakazi wanne wa Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai waliokuwa wanashikiliwa tangu Juni 7,
mwaka huu. Rais wa mahakama hiyo, Jaji Sang-Hyun Song amepongeza uamuzi
huo, kwani utawawezesha wafanyakaizi hao kuungana na familia zao.
Wafanyakazi hao walikamatwa walipoenda kumtembelea Saif Al-Islam Gaddafi
anayeshitakiwa na mahakama hiyo kwa uhalifu dhidi ya binadamu.
WIKI IJAYO
Lubanga kuhukumiwa: Jumanne ijayo, Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai itatoa adhabu dhidi ya aliyekuwa kiongozi
wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia yaCongo, Thomas Lubanga, ambaye
ameshatiwa hatiani kwa makosa ya uhalifu wa kivita kwa kuwasajili na
kuwatumia watoto kwenye vita katika Wilaya ya Ituri nchini humo kati ya
Septemba 1, 2002 na Ogasti 13, 2003.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia