NMB YASAIDIA WANAFUNZI SAME
Meneja wa
huduma kwa wateja wa benki ya NMB tawi la Same , Anna Efrem (kushoto) akikabidhi
zawadi kwa mwanafunzi Omari Silayo baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kwa
wanafunzi wa shule ya msingi Majengo iliyopo wilayani Same,kujibu maswali vizuri juu ya ufahamu wa
masuala ya kibenki kuhusu mpango wa NMB Financial Fitness uliozinduliwa na
benki hiyo kwa watoto wilayani humo.
Benki ya NMB wilayani Same imefanikiwa kwa kiwango
kikubwa kutoa elimu ya mpango wa uelewa wa masuala ya fedha(Financial Fitness)
kwa watoto wa shule za msingi uliozinduliwa hivi karibuni ambao umewajengea
uwezo watoto kuhifadhi fedha mahali salama tangu wakiwa na umri mdogo.
Meneja wa huduma kwa wateja wa NMB tawi la Same , Anne
Efrem alibainisha hayo wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango huo uliofanyika katika shule ya msingi
majengo na kuwashirikisha wanafunzi mbalimbali wa shule za msingi kutoka
wilayani humo.
Alisema mpango huo utasaidia watoto kuwa na
tabia ya kuhifadhi fedha benki wakiwa na umri mdogo bila kuwa na matumizi
mabaya ,hali ambayo itasaidia kupunguza upotevu ovyo wa fedha na kuwataka
watoto hao kuitoa pia elimu hiyo kwa wazazi wao.
Efrem alifafanua kuwa mkakati wa benki ya NMB ni
kuufikisha mpango huo kwa jamii nzima wakianzia na watoto na baadae kuufanya
kila mmoja kuwa na uelewa wa masuala ya kibenki katika kutumia fedha kwa
uangalifu.
Aidha alisema benki ya NMB kupitia sera yake ya
msaada kwa jamii ambayo ipo kwa ajili ya mambo matatu,Afya,Elimu na Michezo
imeanzisha mpango huo unaofanyika nchi nzima kwa kujikita zaidi kutoa elimu
hiyo kwa watoto waliopo kwenye shule za msingi hapa nchini.

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia