16 BORA COPA COCA-COLA KUANZA J’MOSI



16 bora ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 inaanza kesho (Julai 7 mwaka huu) kwa mechi nne zitakazokutanisha timu nane kati ya 16 zilizofuzu hatua hiyo. Mechi hizo za 16 bora zitachezwa kwenye viwanja vya Kumbukumbu ya Karume na Tanganyika Packers vya Dar es Salaam.
 
Ruvuma iliyoongoza kundi A itacheza na Temeke iliyoshika nafasi ya tatu kundi C. Mechi hiyo itaanza saa 2.30 asubuhi Uwanja wa Karume. Mechi nyingine ya asubuhi itakayochezwa Tanganyika Packers itawakutanisha washindi wa pili kundi A Kigoma dhidi ya Mara walioshika nafasi ya nne kundi C.
 
Mechi za jioni kwa kesho zitakazoanza saa 10 kamili jioni zitakuwa kati ya Mjini Magharibi na Kagera kwenye Uwanja wa Karume wakati Morogoro na Pwani zitaumana kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
 
Hatua ya 16 bora itakamilika keshokutwa (Julai 8 mwaka huu) kwa mechi za asubuhi kati ya Kinondoni na Rukwa kwenye Uwanja wa Karume, na Dodoma dhidi ya Arusha kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers. Mechi za jioni siku hiyo ni kati ya Kilimanjaro na Mwanza (Uwanja wa Karume) na Tabora na Tanga (Tanganyika Packers).
 
Timu zitakazoshinda zitaingia hatua ya robo fainali itakayochezwa Julai 10 na 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Nusu fainali itachezwa Julai 13 mwaka huu, na kufuatiwa na mechi ya mshindi wa watatu na fainali ambazo zote zitachezwa Julai 15 mwaka huu.
 
SABA WAPATA ITC KUCHEZA KENYA, MSUMBIJI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa Watanzania saba kucheza mpira wa miguu katika nchi za Kenya na Msumbiji.
 
TFF imetoa hati hizo kwa wachezaji hao baada ya kuombewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Msumbiji (FMF) ili waweze kucheza katika klabu za nchi hizo.
 
Wachezaji waliokwenda Bandari ya Kenya na klabu walizokuwa wakichezea nchini kwenye mabano ni David Naftali (huru), Meshack Abel (huru), Mohamed Banka (huru) na Thomas Mourice (Mtibwa Sugar).
 
Klabu ya CD Madchegde ya Msumbiji imewachukua wachezaji Hassan Hassan Mustapha kutoka Mgambo Shooting ya Tanga, na Abdallah Ally Abdallah na Thobias David Silas kutoka klabu ya daraja la kwanza ya Transit Camp ya Dar es Salaam.
 

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia