ADAI MWENDESHA MASHITAKA KAJICHANGANYA USHAHIDI KESI YA NGIRABATWARE
Timu
ya utetezi katika kesi inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Mipango wa
Rwanda, Augustin Ngirabatware, Jumanne iliiomba Mahakama ya Kimataifa ya
Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) kuzikataa hoja za mwendesha
mashitaka anazodai kumwunganisha mteja wake na mauaji ya kimbari ya
mwaka 1994.
‘’Mwendesha
mashitaka amevurunda ushahidi wake mwenyewe kwa kutoa madai ambayo
hayaungwi mkono na ushahidi wowote,’’ alisema Wakili Kiongozi, Mylene
Dimitri mbele ya Mahakama iliyokuwa inaongozwa na Jaji, William Sekule.
Wakili
huyo alikuwa anatoa hoja za mwisho kupitia mtandano wa video kutoka
nchini Canada. Alidai kwamba baadhi ya mashahidi wa mwendesha mashitaka
nao walikuwa watuhumiwa hali ambayo iliwafanya watoe ushahidi kupata
upendeleo fulani.
Kwa
mujibu wa wakili huyo, mashahidi wa aina hiyo walidanganya na kutunga
ushahidi dhidi ya mteja wake ili wapate adhabu ndogo au kuachiwa toka
gerezani.
Aliulaumu
pia upande wa mwendesha mashitaka kwa kudai kuwa Ngirabatware alihusika
na uhalifu uliofanywa na wanamgambo wa Interahamwe. Alifafanua kwamba
mteja wake hakushitakiwa kwa makosa ya kuwa na mamlaka juu ya
Interahamwe.
Waziri
huyo wa zamani anashitakiwa kwa kula njama za kufanya mauaji ya
kimbari, mauaji ya kimbari au kushiriki mauaji hayo, uchochezi,
kuteketeza kizazi na ubakaji kama uhalifu dhidi ya binadamu.
Uwasilishaji wa hoja za mwisho unaendelea Jumatano.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia