TAASISI YA KURITHI KAZI ZA ICTR YAZINDULIWA RASMI
Rais wa Taasisi ya Kimataifa itakayorithi kazi za Mahakama ya
Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (MICT),Jaji Theodor Meron
Jumatatu ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za pamoja
katika kuwasaka na kuwatia mbaroni watuhumiwa wa mahakama hiyo ambao
bado hawajakamatwa akiwemo Felicien Kabuga anayesadikiwa kuwa kinara wa
mauaji hayo.
“Taasisi hii haina budi na itafanyakazi na nchi mbalimbali
duniani kuhakikisha kwamba washitakiwa hao wa ICTR wanaletwa mbele ya
haki. Hatuwezi kuwaachia washitakiwa hao wa makosa mazito kabisa kuwa
nje ya mkondo wa sheria,’’ alisisitiza Rais wa MICT,Jaji Theodor Meron,
wakati wa sherehe ya uzinduzi wa chombo hicho.
‘’Kama Rais wa Taasisi hii, naahadi
kufanya kila ninaloweza kwa kushirikiana na mwendesha Mashitaka (Hassan
Bubacar) Jallow kuhakisha kwamba nchi zinashirikiana nasi kuwakamata na
kuwashitaki watuhumiwa waliobaki,’’ alisema.
Taasisi hiyo ya MICT inachukua kazi muhimu zitakazokuwa zimebakia
kukamilishwa na ICTR na Mahakama nyingine ya Kimataifa ya Uhalifu ya
Kivita katika Yogoslavia ya zamani (ICTY).
Washitakiwa wengine wawili ambao pia wamepangwa kushughulikiwa na
MICT ni pamoja na Waziri wa zamani wa Ulinzi, Augustin Bizimana na
Kamanda wa zamani wa kikosi cha Walinzi wa Rais, Protais Mpiranya.
Kiongozi huyo wa MICT pia alisema kwamba atatekeleza kazi nyingine
zilizopewa taasisi yake ikiwa ni pamoja na ulinzi wa waliathiriwa na
uhalifu huo pamoja na mashahidi,uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu na
kusimamia utekelezaji wa adhabu kwa waliotiwa hatiani.
Kwa mujibu wa Jaji Meron MICT itashughulikia pia maombi ya wafungwa watakaoomba kuachiwa huru mapema kwa msamaha.
Jaji huyo alitumia nafasi hiyo pia kuishukuru serikali ya Jamhuri ya
Muungano waTanzaniakwa kuipatia eneo la kujenga ofisi za MICT mjini,
Arusha, ambako nyaraka na kumbukumbu za ICTR zitahifadhiwa.
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi huo, Mwendesha Mashitaka wa
MICT, Hassan Bubacar Jallow, alisema, watuhumiwa wengine sita waliobakia
na kesi zao kuhamishwa kwenda kusikilizwa nchini Rwanda hawatasemahewa
kwani nao wataendeelea kusakwa vikali, kwani kinyume chake itakuwa ni
sawa na kushindwa kwa mfumo wa utendaji haki wa kimataifa.
‘’Juhudi za mfumo wa haki wa kimataifa utakuwa unaathiriwa
vibayakamaviongozi hao wa mauaji ya kimbari hawatakamatwa na
kuwajibishwa kwa vitendo vyao,’’ alisisitiza.
Washitakiwa hao sita ni pamoja na luteni kanali mmoja, mameya watatu, inspekta wa zamani wa polisi na mmiliki wa mgahawa mmoja.
Sherehe ya uzinduzi wa MICT imehudhuriwa na viongozi mbalimbali
mashuhuri wakiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
anayeshughulikia Kitengo cha Sheria, Stephen Mathias, Waziri wa Sheria
na Katiba wa Tanzania, Mathias Chikawe, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa
Rwanda, Martin Ngoga, Rais wa ICTR, Jaji Vagn Joensen pamoja na majaji
wengine wa ICTR na wafanyakazi.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia