BREAKING NEWS

Wednesday, April 10, 2013

MUNGAYA.NIMEONEWA ,MIMI SIYO MLINZI WA MBOWE

Mwenyekiti wa Uvccm wilaya ya Arumeru mkoani Arusha aliyesimamishwa kwa muda ili kupisha uchunguzi,Boniphace Mungaya(picha na moses mashalla

SAKATA la kusimamishwa mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),wilaya ya Arumeru mkoani Arusha,Boniphace Mungaya limeonekana kuvuta hisia mbalimbali kwa wanasiasa, vyombo vya habari na viunga mbalimbali vya mkoa wa Arusha.
Mungaya,alisimamishwa mnamo oktoba mwaka jana ili kupisha uchunguzi baada ya kuandikiwa barua na katibu wa CCM mkoani Arusha,Mary Chatanda huku akituhumiwa kwamba ni mlinzi wa mwenyekiti wa Chadema taifa,Freman Mbowe madai anayoyapinga vikali.
Hivi karibuni mwandishi wa gazeti hili alikutana uso kwa uso na kada huyo wa CCM na kisha kufanya mahojiano naye kuhusu sakata hilo.
SWALI.Je umepokeaje uamuzi wa kusimamishwa ndani ya chama chako?
JIBU.(anavuta pumzi)…..Kwa kweli huu ni unyanyasaji  ndani ya chama sijui baya nililolifanya waliniandikia barua ya kunisimamisha uongozi kwamba nimefanya usaliti ndani ya chama kwamba mimi ni mlinzi wa Mbowe na nimeonekana naye mkoani Mtwara kwenye M4C jambo ambalo si la kweli kabisa.
Hata siku moja sijawahi kuhudhuria mkutano wa Chadema,na tena sijawahi kupata bahati ya kufika mkoani Mtwara,jambo hili halina uhakika na hakuna hata ushahidi wa picha ukweli ni kwamba nimefananishwa na mlinzi wa Mbowe aitwaye Zachariah Swai.
Mara nilivyopokea barua ya kusimamishwa sikuchukua hatua yoyote kwani nasubiri uamuzi  na taratibu ndani ya chama hadi sasa kwani walinisimamisha tangu oktoba mwaka jana.
Vijana wengi Arumeru walionichagua hata wale ambao hawakunichagua ninajitahidi kuwatuliza hakika nawambiwa wasubiri uamuzi wa chama kwa kuwa wengi kila siku wanauliza nini hatma yangu ndani ya CCM.
Sisi tunaongozwa na kanuni na taratibu ndani ya chama hizi ni changamoto tunazozipitia sisi vijana ndani ya chama kama mimi kusimamishwa vijana wengi wamesononeshwa sana katika hili jambo langu wengi wameona ni uonevu.
Hadi sasa nina imani kubwa na kamati ya siasa mkoa wa Arusha kwamba itanirejeshea nafasi yangu ,nina imani hiyo kwamba hivi punde watanirejesha madarakani na haki itatendeka pasi na shaka.
SWALI.Endapo ikitokea kwamba umevuliwa uongozi je utachukua hatua gani?
JIBU.Sitahama chama changu mimi si kama wengine wanavyofanya pindi wanapovuliwa madaraka,nitaendelea kusimama ndani ya chama change  kama kada wa kawaida kwa kuwa sioni sababu ya kuhama kwenda kwingine.
Unajua ndani ya chama change kuna sera nzuri zinazotekelezeka ambazo huwezi kuzipata kwingine msimamo wangu ni kwamba nitaendelea kubaki mwanachama hai wa CCM hata wakinivua madaraka.
 
SWALI.Madai ya vijana ndani ya vyama vya siasa nchini kutumika kama madaraja ya kupitisha wagombea unayazungumziaje?
JIBU…..(anacheka kidogo)……sio vyema kuwatumia vijana kama madaraja au mipira ya kiume(condoms),tabia ya kuwatumia wakati wa uchaguzi au nyakati nyingine sio njema kabisa huu ni unyanyasaji na uonevu mkubwa ni vyema  kuwakumbuka vijana wakati kiongozi unapopata madaraka.
Hii tabia ndiyo imewacost(imewagharimu) baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wengi walipiganiwa  lakini mwisho wa siku wakajisahau na sasa wamewatupa vijana baada ya kuwatumia hivyo ushauri wangu ni kwamba si vyema kuwatumia vijana kama madaraja ya kupata nafasi na kisha kuwatupa.
SWALI.Je una mtizamo gani kwa vyama vya upinzani hapa nchini?
JIBU.Upinzani kwangu hauna shida yoyote kabisa,ila ninataka viongozi kutoka vyama vya upinzani watekeleze majukumu ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwa wanasiasa wote tunahudumia jamii zetu.
Upinzani sio vurugu,upinzani sio matusi wala fujo ukiwa mpinzani ukatawala kwa  vurugu haziwezi kusaidia  nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo lakini kwa hali ya sasa naona upinzani umekuwa ni vurugu tu.
Kwa mfano kwetu Arumeru kuna baadhi ya kata zimeshikiliwa na wapinzani lakini sasa hivi wananchi wanalalamika kwamba hazifanyi vizuri kimaendelea kisa wananchi walipiga kura za chuki tu hivyo upinzani sio vurugu ni maendeleo.
SWALI.Je unadhani CCM kitang”oka  madarakani mwaka 2015?
JIBU….(anacheka tena)…Hata siku moja hakuna kitu kama hicho ,CCM  ndiyo inazidi kushika chati ndiyo inazidi kufanya kazi lakini pia ndiyo inazidi kung”aa .
Wote wanayoiombea ife watabaki kuomba hadi kesho ifike lakini haitafika ,kwa kuwa sasa hivi CCM tuna umri wa kutosha tangu kizaliwe na tuna sera zinazotekelezeka ambazo huwezi kuzipata mahali kwingine,kwa kweli bado sijaona mbadala wa kuing”oa CCM hadi sasa.
SWALI.Je una matarajio gani ya kisiasa hapo baadaye?
JIBU.Kwanza ni kukisimamia chama changu na kushirikiana nacho bega kwa bega kutekeleza ilani yake kwa kuwa CCM ndiyo tunasimamia serikali   lakini pia kusimamia haki na wajibu ndani ya chama changu siku zote.
Lakini kuwatumikia vijana wa CCM Arumeru pamoja na wananchi wote bila itikadi zao,ninatarajia kutowaangusha  vijana wenzangu kwani nitaendelea kusimamia haki ndani ya chama changu kwani nina imani nacho na vijana wasiogope kwani mimi ndiye mwenyekiti wao hakuna mwingine.
SWALI.Mbali na nafasi ya uenyekiti je umeshawahi kushika nafasi yoyote?
JIBU.Nimeshika nafasi mbalimbali tu tangu nikiwa chipukizi ndani ya CCM mwaka 1994 nikiwa mwenyekiti wa chipukizi kata ya Kiranyi na baadaye nikawa mwenyekiti wa tawi  kisha baadaye nikachaguliwa kuwa mjumbe wa baraza la wilaya ya Arumeru mwaka 2005 hadi 2010.
Nimekuwa mwenyekiti wa Uvccm kata ya Kiranyi hadi sasa,mwenyekiti wa mtaa wa Sakina , ni  mjumbe wa serikali ya kijiji cha Kiranyi   lakini pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya.
Ieandika na Moses Mashalla,

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates