WAKATI
Aprili 12 mwaka huu Watanzania wanatimiza miaka 29 tangu Waziri Mkuu
aliyeweka historia ya pekee nchini, Edward Moringe Sokoine alipofariki
dunia kwa ajali ya gari, mwili wake umehamishwa kutoka kwenye kaburi la
awali na kuzikwa katika kaburi jipya, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Habari kutoka kwa ndugu wa karibu wa marehemu Sokoine,
zililiambia gazeti hili kuwa mwili wa waziri mkuu huyo ulizikwa kwenye
kaburi jipya mwishoni mwa mwaka jana mjini Monduli.
Kwa mujibu wa
habari hizo, mwili wa Sokoine umezikwa upya baada ya kaburi lake la
awali kupasuka na kuharibika kutokana na tetemeko la ardhi lililotikisa
milima ya Oldonyo Lengai mwaka jana na kusababisha maji kuingia ndani.
Mmoja
wa watoto wa kiongozi huyo wa zamani, aliliambia gazeti hili kuwa baada
ya kaburi hilo kuharibika na kuchakaa, Rais Jakaya Kikwete aliagiza
lijengwe upya.
“Lilipasuka kiasi kwamba ukimwaga maji yalikuwa
yanaingia hadi ndani. Rais Kikwete aliagiza lijengwe upya na baadaye
walitumwa wanajeshi ambao pamoja na ndugu tulikubaliana kuchimba kaburi
jipya na kuhamishia mwili huo katika kaburi jingine,” alisema mtoa
habari wetu.
Kwa mujibu wa habari hizo, shughuli za kuhamisha
mabaki ya mwili huo na kuuzika upya katika kaburi jingine ilifanyika saa
saba usiku na kushuhudiwa na watoto wote na baadhi ya ndugu wa marehemu
walioko ndani na nje ya nchi.
Pia baadhi ya viongozi, akiwamo Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa walikuwapo.
Inaelezwa
kuwa mwili huo uliozikwa ndani ya jeneza miaka 29 iliyopita bila
kufukiwa na udongo, bado uko katika hali nzuri kabisa na hii inatokana
na sindano aliyochomwa ambayo ina uwezo wa kuhifadhi mwili huo katika
hali nzuri ndani ya miaka takriban 40.
“Sanduku lake bado zito na
mwili upo kama ulivyokuwa wakati ule anaagwa. Tulitaka kuufungua na
kuhamishia kwenye jeneza jingine la kisasa tuliloandaa, lakini mzee
Lowassa ambaye ni baba yetu, alituzuia,” alisema mtoa habari wetu.
Alisema
hivi sasa kaburi la awali alimozikiwa limefukiwa na kaburi jipya lipo
jirani na lile la zamani likiwa katika hali na mwonekano mzuri.
Katika
hali ya kushangaza, watoto wa marehemu Sokoine pamoja na baadhi ya
ndugu bado wanakusudia kufanya uchunguzi upya wa mwili huo ili kubaini
kama kweli kifo chake kilitokana na ajali aliyoipata au la.
Ikumbukwe
kuwa wakati wa kifo chake kulikuwa na mjadala mzito, wengi wakidai
aliuawa na kwamba kifo chake kilipangwa na mahasimu wake ndani na nje ya
serikali ambao walikerwa na operesheni yake ya kupambana na wahujumu
uchumi na mali za taifa.
Kwa mujibu wa habari hizo, wapo baadhi
ya watoto na ndugu wanaoamini kuwa kwa jinsi msafara wa kiongozi mkubwa
kama waziri mkuu unavyowekewa ulinzi, ni vigumu gari jingine kutoka
upande wa pili na kuligonga gari lake, hivyo wanaamini aliuawa.
“Siku
tuliyozika upya, ndugu wote tulikubaliana mwakani tuombe kibali cha
serikali kuleta wataalamu kuchunguza ili kubaini chanzo cha kifo chake
kama kilitokana na ajali au la.
“Lakini mzee Lowassa alituzuia,
na kwa vile tunamheshimu sana kama baba yetu tuliukubali ushauri wake,
lakini mwakani tumepanga tuufanyie uchunguzi mwili huo,” alisema mtoa
habari wetu.
Kwa mujibu wa sheria, mwili ukishazikwa unaruhusiwa
kufanyiwa uchunguzi baada ya miaka 30 na mwakani mwili wa Sokoine
utafikisha umri wa miaka 30 tangu ulipozikwa na huo utakuwa muda muafaka
kwa wana ndugu hao kutaka kujua ukweli wa kifo cha ndugu yao.
Sokoine alifariki dunia Aprili 12 mwaka 1984 eneo la Wami-Dakawa akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Ilikuwa majira ya saa kumi jioni, Mwalimu Julius Nyerere alipotangaza kifo chake kwa sauti ya huzuni.
Sokoine alikuwa kiongozi wa kweli ambaye daima alisimama upande wa umma.
Wengi wanamuelezea kwamba alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa kwani aliishi kama alivyohubiri.
Sokoine
si tu kwamba hakujilimbikizia mali, bali pia alipunguza hata mali zake
ili apate nafasi zaidi ya kuwatumikia Watanzania.
Itakumbukuwa
kwenye kikao cha Bunge cha mwezi Aprili 1984, Sokoine alikabiliana na
hoja za wabunge kutaka kuongezewa posho na marupurupu yao ambapo
alitamka: “Ndugu Spika, niko tayari kuwaongezea wabunge posho ya chakula
chao, lakini kamwe sitakuwa tayari kuwaongezea mishahara na marupurupu
mengine.”
Baada ya kikao kile cha Bunge, Sokoine badala ya
kupanda ndege ya serikali kumrudisha Dar es Salaam, aliamua kurudi kwa
njia ya barabara, apate nafasi ya kuona shughuli za maendeleo.
Tanzania Daima
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia