Jamii nchini imetakiwa kuwa na mshikamano
upendo na kudumisha amani iliyopo ambayo imeachwa na waasisi wa Taifa la
Tanzania bila kujali dini,kabila wala itikadi au ubaguzi wa aina yoyote ile.
Hayo yalielezwa juzi na Mwenyekiti wa kikundi
cha Muungano cha Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara,Daudi
Ogori baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo.
Ogori alisema watanzania wanapaswa kuendeleza
amani na upendo uliopo nchini,ambayo ni tunu iliyoachwa na waasisi wa Taifa
kuliko kuendeleza chuki na mifarakano ambayo haina sababu za msingi.
Katika uchaguzi huo Ogori alichaguliwa kuwa
Mwenyekiti kwa kupata kura 196 dhidi ya Odianya Suke aliyepata kura 158 na
Makamu Mwenyekiti alishinda Msiem Ondere aliyepata kura 200 na Gay Abiti
alipata kura 120.
Nafasi ya Katibu mkuu,ilikamatwa na Mtaalam
Nyang’ore aliyepata kura 200 dhidi ya Fred Oguti aliyepata kura 120 katika
uchaguzi huo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.
Wakizungumza baada ya kupata nafasi
hizo,viongozi hao waliwashukuru wanachama wa kikundi hicho kwa kuwapa nafasi
hizo na waliahidi kutumika kwenye nafasi hizo kadiri ya uwezo wao.
Walisema kuongoza ni dira hivyo nao watatumia
nafasi hiyo kwa ajili ya kuongoza kikundi hicho na jamii kwa ujumla huku
wakitanguliza mbele maslahi ya wanakikundi waliowapa dhamana kubwa ya
kuwachagua.