Afisa Mnadhimu namba wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi
wa Polisi (ACP) Japhet Lusingu akitoa ufafanuzi wa mada mbalimbali
zilizojadiliwa kati ya Jeshi hilo na wadau wa Polisi Jamii Mkoa wa
Arusha katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Bwalo la Afisa wa Polisi
(Police Officers Mess) mwishoni mwa wik
Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Francis Duma
akitoa elimu ya Polisi Jamii katika kikao kilichowajumuisha viongozi wa
Jeshi la Polisi na Wadau wa Polisi Jamii Mkoa wa
Arusha.
Katibu wa kikao cha Viongozi wa Polisi na Wadau wa Polisi Jamii ambaye
pia ni Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Arusha Bw. Adolph Olomi akitoa
mwongozo kwa wadau juu ya uendeshaji wa kikao hicho kilichofanyika
Ukumbi wa Bwalo la Polisi mwishoni mwa wiki.
Mdau wa Polisi Jamii ambaye pia nin Mwanasheria wa Halmashauri ya Jiji
la Arusha Bw. Kiomoni Kibamba akisisitiza jambo wakati anachangia mada
ya Usalama mkoa wa Arusha katika kikao kilichofanyika Ukumbi wa Bwalo la
Polisi mwishoni mwa wiki iliyopita
Picha ya pamoja kati ya baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa
Arusha na wadau wa Polisi Jamii mkoani hapa mara baada ya kikao cha
kujadili usalama kilichofanyika ukumbi wa Bwalo la Polisi habari picha na woindeshizza blog
Wadau wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha kutoka kada mbalimbali
wakiwemo wanasheria, wafanyabiashara na wafanyakazi kutoka sekta binafsi na za
kiserikali wamedhamiria kufungua Akaunti benki kwa ajili ya kuliwezesha Jeshi
la Polisi katika kupambana na uhalifu.
Hayo yalielezwa na wadau hao wakati wa kikao cha kujadili
usalama wa mkoa huu kilichofanyika kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi (Police
Officers Mess) mwishoni mwa wiki kati yao na Viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani
hapa. Wadau hao walisema kwamba wawezeshaji wa Jeshi hilo ni wana Arusha
wenyewe hakuna mtu yeyoye atakayetoka mkoa mwingine kwa ajili ya kuliwezesha
Jeshi la Polisi mkoani hapa.
“Tunataka Arusha iwe mfano na mikoa mingine iige, bila
kuwawezesha Polisi hatuwezi kukomesha uhalifu na tunatakiwa tuwawezeshe ili
tupate nafasi ya kuwalaumu, hivyo basi nashauri iundwe Kamati ndogo
itakayowajumuisha Polisi na Wananchi ambao watafanya harambee kwa watu
mbalimbali”. Alisema Kiomoni Kibamba ambaye ni Mwanasheria wa Halmashauri ya
jiji la Arusha.
Wadau hao walisema pamoja na Mfuko huo kutumika kuliwezesha
jeshi la Polisi katika kuongeza bajeti ya mafuta na vifaa vingine lakini pia
utakuwa unatumika kuwapa motisha wale wote watakaokuwa wanaliwezesha Jeshi hilo
kuwapa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuonyesha kuwa wanathamini mchango
wao.
Mbali na mada mbalimbali zilizokuwa zinajadiliwa siku hiyo
pia wadau hao walilishauri Jeshi la Polisi Mkoani hapa kuwa makini na waendesha
pikipiki yaani Boda Boda na ikibidi kila pikipiki inayotumika kusafirisha
abiria iwe na makazi ya maegesho yanayojulikana ili tukio la uhalifu
linapotokea askari wawe wanapata pa kuanzia katika suala zima la upelelezi.
Walisema kwa sasa pikipiki hizo zinafanya kazi mpaka usiku
hivyo kama kuna uwezekano wangewekewa ukomo hasa muda wa usiku badala ya kufanya
biashara hiyo mpaka asubuhi kwani baadhi yao wanatumia mwanya huo na kujiingiza
katika vitendo vya kihalifu.
Awali akifungua kikao
hicho Katibu wa kikao hicho Bw. Adolph Olomi ambaye pia ni Mwenyekiti wa TCCIA
mkoa wa Arusha, alisema kwamba pamoja na mambo mengine lakini pia lengo la
mkutano huo ni kufahamiana ili kupunguza kama si kuondoa kabisa pengo kati
Jeshi hilo na wananchi hali ambayo itasaidia kuwa na ukaribu utakaosaidia
kushughulikia matatizo ya kihalifu kabla hayajatokea.
Kwa upande wake Afisa Mnadhimu namba moja wa Jeshi hilo
mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Japhet Lusingu aliwataka wadau
hao watoe taarifa za wahalifu na uhalifu kupitia kwa viongozi wa Jeshi hilo ili
kupunguza malalamiko juu ya uvujaji wa taarifa hizo.
(ACP) Lusingu aliongeza kwa kusema kwamba, hata watoa taarifa
mara baada ya kutoa taarifa Polisi wanatakiwa wakae kimya bila kumshirikisha mtu
yeyote kwani hali hiyo inasababisha
majirani kumfahamu mtoaji wa taarifa hizo na baadae wahalifu kumfahamu kisha
lawama kuliangukia jeshi la Polisi hivyo akasisitiza kwamba usiri unatakiwa
kuanzia kwa mtoa taarifa mwenyewe.
Akitoa mada katika kikao hicho Mkuu wa kitengo cha Polisi
Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi (SSP) Mary Lugola alisema kwamba,
umefika wakati muafaka kwa Jeshi la Polisi na wananchi wote kufanya kazi kwa
ukaribu zaidi ili kuweza kuimarisha usalama. Alisema kikao hicho ni moja ya
mpango mkakati wa kuhakikisha mkoa wa
Arusha unakuwa salama hasa ikizingatiwa pia ni kitovu cha shughuli za kitalii.
Naye Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu wa Polisi (SP)
Francis Duma alisema kwamba, Falsafa ya Polisi Jamii ilikuja baada ya kuona
kuna pengo kubwa kati ya Polisi na Jamii hivyo kuondoshwa kwa pengo hilo
kumesaidia pande hizo mbili kuwa karibu.
Alisema Polisi pekee bila kushirikiana na wananchi haiwezi
kukomesha uhalifu ikizingatiwa kwamba, kutokana na sensa ya mwaka 2012 uwiano
unaonyesha kuwa, Polisi mmoja anatakiwa ahudumie kaya 1300 kwa masaa 24 bila
kupumzika, hivyo ukomeshaji wa matukio ya uhalifu utafanikiwa endapo wanajamii
nao watajitoa ipasavyo katika suala zima la kuimarisha usalama
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia