Mjumbe
wa Bunge la Katiba, Ali Mohamed Kessy ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi
Kaskazini (CCM) akiwatangazia waandishi wa habari kuunga mkono muundo wa
serikali tatu uwepo katika Katiba Mpya, mjini Dodoma jana. Katikati ni
Mwenyekiti wa Kamati namba moja ya bunge hilo, Ummy Mwalimu na Makamu
wake, Prof Makame Mbarawa ambao walimwita Kessy kumtaka kukanusha kuhusu
taarifa yake ya kuwapo tatizo la akidi kwenye vikao vya kamati.
Ilikuwa kama sinema pale viongozi wa Kamati Namba Moja ya Bunge Maalumu
walipojikuta wakibishana na mjumbe wao mbele ya waandishi wa habari,
huku siri za mambo ya ndani ya vikao zikianikwa hadharani.
Kamati
hiyo inaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu
na makamu wake ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame
Mbarawa, huku ikiwa imesheheni vigogo wengine wakiongozwa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda.
Viongozi
wengine katika kamati hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uhusiano na Uratibu), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
Wamo pia
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, Waziri wa Kazi na
Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto, Dk Pindi Chana.
Jana
asubuhi, Mwalimu na Profesa Mbarawa walifika mbele ya waandishi wa
habari katika Hoteli ya St Gasper wakiwa wameambatana na mmoja wa
wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM),
Ally Keissy.
Lengo la
mwenyekiti na makamu wake lilikuwa ni kumbana Keissy ili akanushe
taarifa aliyoitoa juzi kwenye moja ya televisheni kwamba kamati hiyo
inaongoza kwa kuvunja kanuni hasa katika suala la akidi ya vikao
kutotimia.
Walipofika
mbele ya waandishi wa habari, Keissy alipewa fursa ili akanushe taarifa
yake, lakini alibadili mada na kuanza kuzungumzia masuala ya muundo wa
Serikali na Bunge, huku akisema yeye ni muumini wa serikali tatu na siyo
mambo ya serikali mbili zinazopendekezwa na wengi kutoka katika chama
chake.
Kauli hiyo iliwashtua Mwalimu na Profesa Mbarawa ambao walianza kumkatisha ili asiendelee.
"Keissy
sikukuitia mambo hayo, huu ni mkutano wangu, naomba ukanushe
nilichokuitia, hayo utazungumza baadaye tafadhali sana," alisema
Mwalimu.
Wakati
huo Profesa Mbarawa na waandishi wa habari waliokuwapo walivunjika mbavu
kwa vicheko, huku yeye akiendelea kusisitiza kwamba ni muumini wa
Tanganyika.
Wakati
akisema hayo, Profesa Mbarawa naye aliingilia kati na kumtaka Keissy
kueleza kilichompeleka hapo huku akimtaka aache kelele za kupotosha
wananchi kwa kuwa anachosema siyo kweli.
Alipopewa
nafasi ya kuzungumzia jambo hilo, Keissy alisema: "Jana, mimi
nilihesabu mara mbili nikaona Zanzibar hawajatimia lakini kumbe mmoja
nilimfanya akawa mtu wa Tanganyika, kwa hilo nilighafilika, lakini mle
ndani mambo siyo mazuri," alisema Keissy.
Kabla
hajaendelea Mwalimu alidakia na kumtaka anyamaze kimya kwa kuwa huo
haukuwa mkutano wake, ili yeye (Mwalimu) aendelee kueleza mambo
yaliyojiri ndani ya kamati.
"Jamani
waandishi si mnaona amekanusha, huu ni mkutano wangu na yeye sitaki
azungumze mambo ya mle ndani kwa kuwa msemaji ni mimi au makamu wangu au
mtu yeyote atakayeteuliwa na mwenyekiti, sasa tunaendelea," alisema
Mwalimu.
Mara
baada ya Mwalimu kutoa taarifa ya kamati yake kwa waandishi wa habari na
kumaliza kujibu maswali, alinong'ona na Profesa Mbarawa na hapo wakampa
nafasi Keissy ili azungumze kwa ufupi mambo yake lakini palepale mbele
yao.
Kauli za Keissy
Akitumia
fursa hiyo, Keissy alisema: "Kuna mambo yanafanywa mle ndani ambayo mimi
na wenzangu wengine tunalazimishwa, hatukubaliani nayo likiwamo suala
la kuizika Serikali ya Tanganyika wakati wa upande wa pili (Zanzibar)
wanapewa nafasi na kunufaika na rasilimali za nchi hii, ndugu zangu huu
ni uonevu."
Alisema
uonevu huo umekuwa mkubwa kwa wabunge wa Tanzania Bara ukilinganisha na
wenzao wa Zanzibar ambao alisema wanakula fedha nyingi za bure ilihali
hawafanyi kazi za Tanganyika.
"Ndugu
zangu, hapa tusidanganyane, we fikiria watu zaidi ya 50 wanatoka kule
Zanzibar na kuja kutuamulia mambo yetu, hii si halali hata kidogo.
Haiwezekani mtu wa Zanzibar akaja kuzungumzia masuala ya Nkasi wakati
hayajui," alisema.
Alisema
kuwa msimamo wake siku zote ni serikali tatu na kwamba hatayumbishwa na
vitisho au jambo la aina yoyote hata kukiwa na kulazimishwa.
Mbunge
huyo alisema kuwa kutakuwa na urahisi wa kuongoza Serikali kama
Tanganyika itapewa hadhi yake kuliko ilivyo sasa kwa serikali mbili
zinazopigiwa upatu.
Kwa
mapendekezo yake alisema ni vyema likawepo Bunge la Tanganyika, Bunge la
Zanzibar na kisha miongoni mwa wabunge hao, wachaguliwe wachache kuunda
Bunge la Muungano.
Aliendelea
kusisitiza kuwa wabunge kutoka Zanzibar wanawanyonya wenzao wa Tanzania
Bara kwa kila kitu kauli ambayo ilionekana kumkera Profesa Mbarawa na
kuamua kumkatisha asiendelee kuzungumza.
Wakati
akiendelea kuzungumza, viongozi hao walimkatisha tena na kumwambia
akubali waondoke pamoja kuendelea na vikao vya kamati. Baada ya hapo,
Mwalimu na Profesa Mbarawa walinyanyuka na kuanza kuondoka, lakini
Keissy alisimama na kuendelea kuzungumza na waandishi wa habari.
Baada ya
kuona anaendelea, Profesa Mbarawa alirudi na kumshika mkono Kessy huku
akisema; "Mheshimiwa Keissy twende bwana, maana ukimwacha huku huyu
atazungumza mambo mengi."
Wakati
akiondoka eneo hilo, Keissy alipaza sauti akiwaambia waandishi wa
habari: "Angalieni tunavyodhibitiwa, lakini msimamo ni huo wala
sitayumba ngoja tukaendelee lakini mimi ndiyo mtoa habari namba moja."
Msimamo wa serikali tatu ni wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) waliosusia Bunge.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia