MADIWANI WAMTAKA MKURUGENZI LONGIDO KUSITISHA MRADI WA MAJI

Baraza la Madiwani wa Halmshauri ya Longido, limetoa tamko kutokana na mgogoro wa mipaka kati ya Wilaya za Longido na Arumeru kwa kumtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Julius Chalya, kusitisha ujenzi wa  mradi wa maji ambao mpaka sasa umegharimu Sh. milioni 200.
Akizungumza katika Baraza la Madiwani lililofanyika katika halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Joseph Ole Sadira, alisema wameamua kutoa tamko hilo kutokana na Halmashauri kuweka alama za mipaka mara tatu mfululizo na alama hizo kutolewa bila mtu yeyote kuchukuliwa sheria.

Hata hivyo, madiwani hao walisema chanzo cha mradi huo kipo wilayani Arumeru, hivyo wana shaka ya kutumia fedha nyingi za wananchi katika kuhakikisha wananchi wa Longido wanapata maji.

“Baraza hili limeamua kutoa tamko kuwa walioshiriki kung'oa alama za mipaka wabainishwe na wachukuliwe hatua za kisheria, gharama zilizotumika katika uwekaji wa alama za mipaka zirudishwe na tunaomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi isaidie kutatua migogoro ya mipaka,” alisema Sadira.

Akisoma taarifa ya mgogoro wa mipaka ya Wilaya za Longido, Arumeru na Monduli, Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira wilayani Longido, Elia Samson, alisema juhudi zilizofanywa na kamati mbalimbali na za halmashauri hiyo kuweka alama mara tatu, bado zimeshindwa kudumu na alama hizo kung’olewa mara baada ya kuwekwa hazijazaa matunda.

“Mei 28, mwaka huu, Kamati ya Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Longido, Arumeru na Monduli, ziliagiza wataalam waendelee kurudisha alama husika ambapo jumla ya Shilingi milioni 3.6 zimetumika kama zilivyoagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kazi ilianza Juni 2, mwaka huu ambapo alama hizo ziling’olewa tena kwa mara ya pili na Mkuu wa Mkoa akaagiza kurejeshwa tena,” alisema Samson.

Hata hivyo, alisema kuanzia Juni 17, mwaka huu hadi Juni 19, mwaka huu, kazi ya urejeshwaji alama hizo ulifanyika lakini Juni 19, mwaka huu majira ya jioni, alama husika ziling’olewa tena na zoezi hilo limesitishwa mpaka sasa kwa sababu za kiusalama kwa wapimaji.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo akiwamo Diwani wa kata ya Longido, Motika Kasosi, wamelaani watu wanaong’oa alama hizo na mpaka sasa hawajachukuliwa hatua yoyote huku halmashauri hiyo ikipoteza fedha za walipa kodi na kusababisha hofu ya kutokamilika kwa mradi mkubwa wa maji.

Kasosi alisema suala hilo la mipaka siyo la kufumbiwa macho kwa kuwa halmashauri hiyo inaweza kutekeleza mradi huo mkubwa wa maji na maji hayo yasiwafikie wananchi wa Longido na hivyo serikali kupoteza bure fedha za walipa kodi.

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Esupat Ngulupa, ameomba serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuingilia kati mgogoro huo kutokana na hatua zilizochukuliwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama kutozaa matunda.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post