WANAWAKE nchini wamehamasishwa kuwanyonyesha maziwa ya mama pekee
watoto wachanga katika saa moja mara baada ya kujifungua hadi miezi
sita bila kuwapa kitu chochote ikiwemo maji na juisi kwa kuwa maziwa
yanachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha maendeleo ya uhai wa mtoto.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine
Ishengoma wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji
duniani kwa wanahabari na kufanyika ukumbi wa Gentle Hill na kitaifa
kufanyika Wilaya ya Mufindi, Katibu Tawala Mkoa, Wamoja Ayubu, alisema
wanahabari wanatakiwa kutumia kalamu zao kuhamasisha jamii kuhusu njia
bora za kumsaidia mama ili aweze kunyonyesha kwa ufanisi pamoja na
kutoa taarifa muhimu zinazohusu ulishaji watoto wadogo hususani
unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Pamoja na hayo, alisema kuwa, asilimia 49 ya wanawake wanaojifungua
ndiyo wanaowaanzishia watoto wao kunyonya maziwa ya mama katika muda
sahihi baada ya kujifungua.
“Takribani asilimia 30 ya watoto wachanga wanapewa maji, vinywaji au
vyakula kabla hawajaanza kunyonyeshwa na asilimia 50 ya watoto ndio
wanaoanzishiwa vyakula vya nyongeza katika umri sahihi wa miezi sita
unaopendekezwa kitaalamu,” alisema Wamoja.
Alisema, unyonyeshaji watoto maziwa ya mama unahimizwa kwa sababu
ni mlo bora, kamili na muhimu kwa mtoto wa binadamu kuliko chakula
kingine katika siku za mwanzo za maisha yake.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFNC),
Mary Kibona, alisema ulishaji watoto maziwa ya mama huchangia katika
kufikia malengo ya milenia kupunguza umaskini uliokithiri na njaa.
Tanzania inaungana na nchini nyingine duniani kuadhimisha wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama, kuanzia Agosti 1 hadi 7.