Na Mwandishi Wetu
KUMEKUCHA! Miss Kinondoni
anayemaliza muda wake, Lucy Tomeka, ametamba ni lazima mrembo wa Redd’s Miss
Tanzania mwaka huu atoke Kinondoni.
Lucy alisema ana uhakika
huo mkubwa kutokana na kuwaona washiriki wa Redd’s Miss Kinondoni na kuona wana
vigezo vyote vya kulitwaa taji hilo.
Mrembo huyo ambaye
atakabidhi taji la Redd’s Miss Kinondoni mwishoni mwa wiki alisema, ana uhakika
huo kutokana na uzoefu alioupata wakati akishiriki Redd’s Miss Kinondoni.
“Taji lazima lirudi
nyumbani, warembo wa Kinondoni kusema kweli wana sifa zote, wana kila aina ya
sifa. Tena mwaka huu naona upinzani ni mkali zaidi kuliko miaka yote, kutokana
na sifa ya warembo hao,” alisema Lucy.
Naye Mratibu wa Redd’s
Miss Kinondoni, Husna Maulid, alisema warembo 20 wanatarajiwa kuchuana Ijumaa
wiki hii ili kumpata mshindi kati yao.
“Ijumaa fitina yote
inaisha, kinachosubiriwa ni siku tu na warembo 20 wapo katika mazoezi makali
kwa ajili ya shindano hilo.”
Shindano la Redd’s Miss
Kinondoni linatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Escape 1 uliopo Mikocheni,
Dar es Salaam huku kukiwa na burudani kali toka Malaika Band inayoongozwa na
Christian Bella.
Taji la Redd’s Miss
Kinondoni kwa sasa linashikiliwa na Lucy Tomeka, ambaye naye alivikwa na
aliyekuwa Redd’s Miss Tanzania, Brigitte Alfred.
Warembo wanaoshiriki
shindano hilo wanatoka vitongoji vya Sinza, Msasani na Dar Indian Ocean, huku
kiingilio kikitarajiwa kuwa Sh 10,000 kwa viti vya kawaida na Sh 30,000 viti
maalumu.
Wadhamini wa shindano hilo
ni Redd’s Original, Kitwe General Traders, CXC Africa, Jambo Leo, Clouds FM,
Michuzi Media Group, Father Kidevu, Greaters Salon, EFM na Mseto.