PINDA APONGEZA SEKTA YA UTALII ARUSHA
Posted by
woinde
on
Monday, August 11, 2014
in
Habari
MATUKIO
|
WAZIRI
Mkuu Mizengo Pinda ameimwagia sifa hoteli maarufu ya Ngurdoto yenye
hadhi ya nyota tano, iliyopo nje kidogo ya jiji la Arusha, kutokana na
kuwa na ukumbi mkubwa wa kisasa wenye uwezo wa kuketisha watu zaidi ya
3,000 kwa wakati mmoja na kueleza kuwa ukumbi huo ni mkombozi kwa sekta
ya utalii nchini.
Aidha alikitaka kituo
cha kimataifa cha mikutano cha Arusha, AICC kuboresha kumbi zake ili
ziendane na wakati huku akitahadharisha kwamba upo uwezekano wa kituo
hicho kukosa mikutano iwapo kitashindwa kuboresha kumbi zake ziwe na
hadhi ya kimataifa.
Kauli hiyo ameitoa
jijini hapa wakati akifungua mkutano wa wadau wa maji unaofanyika katika
ukumbi huo huku akitumia muda mwingi kutazama mandhari ya ukumbi huo.
"Kwa kweli hili jengo
ni la kisasa sana nimetembea sehemu nyingi hapa nchini sijawahi kuona
ukumbi wa kisasa kama huu, kwa kweli Mrema (mmiliki wa hoteli) ametuokoa
sana, hii ni changamoto kwa AICC wajitahidi kuboresha kumbi zao
vinginevyo watapigwa mweleka,"alisema Bw.Pinda.
Pinda aliongeza kuwa
Tanzania kuwa na ukumbi wa kisasa kama huo ni heshima kwa taifa na hivyo
serikali itajitahidi kuleta mikutano ya kutosha.
Awali mkuu wa mkoa wa
Arusha, Magesa Mulongo, alimweleza Waziri Mkuu Pinda kwa kuitaka
serikali iangalie uwezekano wa kuhamishia mikutano mingi mbalimbali ya
kitaifa na kimataifa kufanyika jijini hapa kwa kuwa tayari inao vigezo
vyote vya kufanikisha mikutano hiyo.
Bw.Mulongo alisema ni
bora mikoa mingine ikakubali kuuachia mkoa wa Arusha kuandaa mikutano
mbalimbali kutokana na vigezo vilivyopo zikiwemo hoteli nyingi zenye
kumbi za kisasa, huku akitolea mfano ukumbi huo wa Ngurdoto maarufu kwa
jina la Tanzania Convention Center.
"Karibuni sana Arusha
yale mambo yetu ya zamani tumeshaacha na wale wanaoamini wangekutana na
mabomu sasa hayapo tena, karibuni kwenye ukumbi mpya wa kisasa zaidi,
mheshimiwa waziri mkuu lazima mikoa mingine wakubali kuuachia mkoa wa
Arusha kuandaa mikutano mbalimbali kwa sababu vigezo vyote
tunavyo,"alisema Bw.Mulongo.
Aidha alisema mkoa wa
Arusha ni kituo cha utalii na vivutio vingi vya kumfanya mgeni afurahie
mandhari yaliyopo hivyo aliongeza kwa kuwataka wadau mbalimbali kuwa
hakuna haja ya kupeleke mikutano sehemu nyingine
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia