Mwenyekiti wa mtandao wa vyombo vya habari vya kijamii Tanzania (COMNETA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa redio FADECO ya wilayani Karagwe, Bw. Joseph Sekiku, akimtambulisha mgeni kutoka nchini Uingereza kwa wamiliki wa redio za jamii katika mkutano uliojadili masuala ya kiufundi uliofanyika mwishoni mwa juma Chuo kikuu huria.(Picha zote na Zainul Mzige).
Na Mwandishi wetu
Kampuni Broadcast warehouse ya Uingereza imesema ipo tayari kusaidia radio za jamii ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto nyingi za uendeshaji hasa katika masuala ya kiufundi kwenye teknolojia ya utangazaji ya digitali.
Mtaalamu wa kampuni hiyo, Brendan Lofty ambaye aliwasili nchini kwa ajili ya mkutano na wanachama mtandao wa vyombo vya habari vya kijamii Tanzania (COMNETA) amesema ipo haja ya kuangalia mfumo wa pamoja wa kiufundi ambao utafanya redio hizo kuwa endelevu.
Alisema anafahamu umuhimu wa radio hizo za jamii ambazo zinaelekeza nguvu kushughulikia matatizo ya jamii kuliko redio za biashara na kusema yupo nchini kuhakikisha anajibu kiu ya wamiliki hao inamalizika na wanaendelea na majukumu yao.
Pichani juu na chini ni baadhi ya wanachama mtandao wa vyombo vya habari vya kijamii Tanzania (COMNETA) ambao ni mameneja na wamiliki wa redio za jamii nchini waliohudhuria mkutano wa siku moja uliojadili masuala ya kiufundi uliofanyika mwishoni mwa juma Chuo kikuu huria.
Alisema katika kuelekea uchaguzi na hasa baada ya TCRA kutoa hadidu za kuzingatiwa inafaa wahusuka wote kuwa katika hali ya kujiamini kwa kuwa na utaalamu unaotakiwa katika kuendesha redio hasa masuala ya kiufundi.
“Nimekuja kuwatoa hofu, tutaelezana na kushauriana namna bora ya kusaidiana kufikia kuwa na redio bora” alisema Lofty.
Alisema katika utafiti wake amebaini kwamba radio za jamii nchini zina kazi kubwa na ya maana kuliko zile za kibiashara na kwamba zipo zenye hali bora zaidi kiufundi kuliko zilizopo Ulaya.
Naye Mwenyekiti wa Comneta, Joseph Sekiku akielezea mkutano huo amesema umeitishwa makusudi kwa ajili ya kupata uzoefu wa mtaalamu huyo wa Uingereza kutokana na redio nyingi kuwa na matatizo ya kiufundi kwenye digitali .
Alisema kutokana na makampuni yaliyouza vifaa mengi kutokuwa na program za kufuatilia vifaa vyao, redio nyingi zimejikuta zikilazimika kununua vifaa vingine walivyonavyo vinapopata hitilafu na hivyo kuongeza mzigo wa uendeshaji.
Alisema wakati Comneta inataka kuwa na uwiano wa ubora wa vifaa na wauzaji wake wameona ni vyema kumuita mtaalamu huyo wa Uingereza ambaye pia kampuni yake inauza vifaa vya radio na digitali kuona namna bora ya kushirikiana.
Aidha alisema hali hiyo imesababishwa na mahitaji halisi ya kuzifanya redio hizo kuwa endelevu na kuendelea kuhudumia jamii hasa kuelekea katika uchaguzi.
Alisema nyingi ya radio hizo hazinahifadhi ya vitu vinavyorushwa kwa siku, hivyo kama masuala hayo yakitatuliwa suala la kufuatilia haki katika mashauri na TCRA yanaweza kuwa na nafuu zaidi.
Mtaalamu kutoka kampuni ya Broadcast warehouse ya Uingereza, Bw. Brendan Lofty, akifafanua masuala ya kiufundi yanayohusu redio na programu zake kwa ujumla kwenye mkutano wa siku moja na wanachama wa COMNETA.
Meneja wa kituo cha redio jamii TUMBATU FM, Bw. Ali Khamis akielezea changamoto mbalimbali za kiufundi wanazokumbana nazo kwenye kituo chake wakati wa mkutano huo na Mtaalamu wa Kampuni ya Broadcast warehouse ya Uingereza, Bw. Brendan Lofty (hayupo pichani).
Mkurugenzi wa redio jamii Uvinza Fm, Alhaji Ayubu Kalufya akiuliza swali kwa mtaalamu huyo Bw. Brendan Lofty(hayupo pichani).
Mtaalamu kutoka kampuni ya Broadcast warehouse ya Uingereza, Bw. Brendan Lofty akibadilishana mawazo na baadhi ya wanachama wa mtandao wa vyombo vya habari vya kijamii Tanzania (COMNETA) wakati wa mkutano huo wa siku moja uliofanyika Chuo Kikuu Huria mwishoni mwa juma.
Maswali yakiendelea kuelekezwa kwa mtaalamu huyo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia