BREAKING NEWS

Friday, December 5, 2014

WADAU WA MADINI WAMPIGIA DEBE WAZIRI MASELE

WAFANYABIASHARA wadogo wa Madini aina ya tanzanite na madini mengine wanaofanya shughuli zao Mtaa wa Pangani jijini hapa wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kumbakiza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele katika nafasi aliyonayo kwani anajali matatizo ya wachimbaji wadogo.
Aidha wamesema endapo Masele akiondolewa katika nafasi hiyo ndoto yao ya kuwa na jengo la kisasa la uuzwaji wa madini hayo litakalojulikana kwa jina la Tanzanite Complex zitakufa.
Walieleza kuwa kwa miaka mingi mawaziri na naibu mawaziri waliohudumu katika Wizara ya Nishati na Madini hawakuwa na ndoto ya kujenga jengo hilo litakalowawezesha wafanyabiashara kuuza madini hayo jijini Arusha.
Wakizungumza jana jijini hapa wafanyabiashara hao walisema wanamuomba Rais Kikwete kumuona Masele kuwa hana hatia na ni kijana mdogo anayefaa kuongoza katika sekta hiyo kwani wachimbaji madini na wafanyabiashara wa madini karibu nchi nzima wanamkubali kwa sababu ya kujali matatizo yao.
Mfanyabiashara wa tanzanite, Godfrey Silvester akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema tangu Masele alipochaguliwa kuwa Naibu Waziri ameweza kukutana na wachimbaji wadogo kutatua changamoto zinazowakabili.
Pia amewasaidia kutoa fursa za ukopaji wa mikopo kupitia Benki ya Rasilimali (TIB) ili kuwawezesha kupata vifaa vitakavyowarahisishia kuchimba madini hayo kisasa zaidi.
“Tunamuomba Rais Kikwete asimtoe Masele katika wadhifa wake kwani ni mtetezi mkubwa kwetu sisi wafanyabiashara na wachimbaji wadogo wa madini ametuonesha njia mbalimbali za kufanya biashara zetu kuwa za kisasa,” alisema Silvester.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates