Huenda yakawa ni mafanikio ya kufungia mwaka katika sekta ya
burudani, baada ya Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Vanessa Mdee ‘Vee
Money’, usiku wa kuamkia jana kutunukiwa tuzo zilizowataja kuwa ni
wasanii bora Afrika Mashariki.
Diamond na Vee Money walishinda tuzo hizo za
kimataifa za All Africa Music Awards (Afrima) zilizotolewa usiku wa
Desemba 27, huko Lagos, Nigeria.
Vanessa alishinda katika kipengele cha Msanii Bora
wa Kike Afrika Mashariki, na kuwashinda Wahu (Kenya), Muthoni The
Drmmer (Kenya), Size 8 (Kenya), Kaz (Kenya) na Jackie Chandiru (Uganda).
Diamond Platnumz alinyakua tuzo ya Msanii Bora wa
Kiume Afrika Mashariki, ambayo alikuwa akiiwania sambamba na Jose
Chameleone (Uganda), Kidumu (Burundi), Maurice Kirya (Uganda) na Peter
Msechu ft Amini (Tanzania).
Msechu alikuwa akiwania tuzo hiyo kupitia wimbo wake ‘Nyota’ aliomshirikisha Amini.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa
Instagram, Msechu alionekana akiwa amebeba tuzo ya Diamond ambaye
hakuhudhuria katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, kutokana na ziara yake
ya kimuziki huko Bujumbura, Burundi ambako alifanya shoo usiku wa
kuamkia leo.
Vee Money ambaye pia ni mtangazaji wa kituo cha
redio cha Choice FM na MTV Base, kupitia ukurasa wake wa Instagram,
aliandika “kwa Mungu kuna utukufu, asanteni sana kwa kunipigia kura.
Ninawapenda ‘Best Female EastAfrica Tanzania.”
Wanamuziki wengine kutoka Afrika Mashariki
waliopata tuzo hizo ni pamoja na Elani kutoka Kenya aliyetajwa mshindi
wa tuzo ya Wimbo Bora wa Pop, huku Radio na Weasel kutoka Uganda,
wakipata tuzo ya Wimbo Bora wa Reggae.
Nigeria waingiwa hofu
Ushindi huo wa kishindo kutoka Tanzania,
umewafedhehesha wanamuziki mbalimbali kutoka Afrika Magharibi, Kusini na
Afrika Mashariki ambao wameonyesha wazi kuanza kuifikiria Tanzania
katika mapinduzi ya muziki kwa mwaka 2015.
Mwanamuziki Davido ameendeleza hofu yake kwa
wasanii wenzake, baada ya kushindwa kumuunga mkono msanii mwenza na
rafiki yake Diamond Platnumz, mara baada ya kutajwa kuwa mshindi wa tuzo
usiku huo.
Tanzania imeanza kung’ara kimuziki dhidi ya mataifa mengine, huku wanamuziki wake wakiwaburuza wenzao wa Afrika Mashariki.